Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya Akiba (ACB) Augustine Akowuah amesema benki hiyo imepata faida ghafi ya Sh. 1.2 bilioni katika nusu ya mwaka iliyoishia ambayo ni sawa na ukuaji wa asilimia 700 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita. Akowuah ameeleza kuwa, ongezeko hilo limetokana na ukuaji wa mikopo iliyofikia Sh. 80 bilioni iliyotolewa kwa wateja takribani 13, 200, wengi wao wakiwa wafanyabiashara wadogo na wa kati.
Mkurugenzi huyo amesema ubora wa mikopo hiyo umetokana na uboreshaji wa taratibu za utoaji wake huku wastani wa mikopo chechefu ukiwa asilimia 0.7 katika kipindi hicho.
“Ninafarijika sana na matokeo haya ya nusu ya pili ya mwaka jana. Mizania ya malengo yetu tangu mwanzo wa mwaka yametusaidia kuwa na muelekeo mzuri wakati tunafunga mwaka. Tunafurahi kwa sababu mikakati mingi tuliyojiwekea imeleta mabadiliko kwenye benki yetu kwa muda mrefu japokuwa hali haikuwa nzuri mwanzoni mwa mwaka”. Amesema Akouwah.
Benki ya ACB ilianzishwa takribani miaka 20 iliyopita na hadi sasa ina matawi katika mikoa mbalimbali kama vile Dar es salaam, Mbeya, Mwanza, Arusha, Moshi na Dodoma