Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Emmanuel Tutuba na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Yusuph Mwenda wamekutana na Wakuu wa benki na Taasisi za Fedha nchini kujadili suala la Hati ya Uwakala katika Ulipaji wa Kodi nchini (Agency Notice).
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika kwenye ofisi za Benki Kuu jijini Dar es Salam Oktoba 17, 2024, Gavana Tutuba amesema lengo la kukutana pamoja kati ya BoT, TRA, Mabenki na Taasisi za Fedha ni kuona namna wanavyoweza kuboresha utendaji wa kazi kwa kushirikiana na kuweka mazingira rafiki ya biashara kwa wananchi bila vikwazo vyovyote.
Tutuba amesema Benki Kuu ya Tanzania itahakikisha inasimamia vyema Taasisi za Fedha na kutatua changamoto zilizopo ili wanaotakiwa kulipa kodi walipe bila kushurutishwa kama Rais wa Jamhuri Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyoagiza.
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu Mwenda amesema kuwa Hati za Uwakala ni njia ya mwisho kabisa ya kukusanya kodi na TRA itaendelea kutoa elimu na kujenga mahusiano ya karibu zaidi na walipakodi ili waweze kulipa kodi zao kwa wakati kwa lengo la kuondokana na matumizi ya Hati hizo za uwakala katika Ulipaji wa Kodi.