Benki kuu ya Tanzania (Bot) imezitaka taasisi ndogondogo za fedha nchini kuwasilisha nyaraka muhimu wanazotumia kufanyia biashara hizo kuanzia wiki ijayo.
Katika taarifa iliyotolewa na Bot Desemba mwaka jana iliwataka wafanyabiashara wa biashara za kifedha ndogondogo kuwasilisha taarifa muhimu za biashara zao hususani kuhusu uendeshaji na umiliki wa taasisi hizo kabla ya January 11.
Miongoni mwa nyaraka muhimu zinazohitajika na Bot ni pamoja na leseni za biashara iliyotolewa na wakala wa usajili wa biashara (Brela),cheti cha utambuzi wa umiliki wa biashara,anuani ya mahali biashara ilipo pamoja na mawasiliano husika,ukaguzi wa hesabu wa kila mwaka,safu ya wamiliki na uongozi wa biashara husika ikiwemo bodi ya wakurugenzi,mtendaji mkuu na uraia wao pamoja na mifumo ya kiteknolojia na mawasiliano,madeni,hisa za wamiliki pamoja na vitega uchumi.
Ikumbukwe bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania novemba mwaka jana lilipitisha sheria ya usimamizi wa huduma ndogondogo za fedha ya mwaka 2018 zinazoipa mamlaka Bot ya kusimamia biashara hizo nchini.