Benki kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza kuwa kuanzia sasa, huduma za kubadilisha fedha za kigeni zitatolewa katika benki pamoja na taasisi za fedha zinazoendesha biashara nchi nzima. Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Benki Kuu, benki na taasisi hizo zinapaswa kutoa huduma hiyo kwa wateja wote.
“Benki Kuu imehimiza benki na taasisi za fedha kuendelea kutoa huduma za kubadilisha fedha za kigeni kwa wateja wote, wakati uchunguzi wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni na maduka bubu unaendelea. Benki Kuu inapenda kuutahadharisha umma kutotumia huduma zisizo rasmi za ubadilishaji wa fedha za kigeni kutokana na hatari mbalimbali zinazotokana na huduma hizo ikiwamo kuibiwa au kupewa fedha bandia”. Imesoma taarifa hiyo.
Aidha, BoT imesisitiza kuwa kutumia huduma zisizo rasmi ni kinyume na Sheria za nchi na kwamba hatua kali zinachukuliwa kwa watakaobainika kutoa na kutumia huduma hizo.