Benki inayokua kwa kasi zaidi nchini Tanzania, FINCA Microfinance imetangaza uzinduzi wa programu ya miezi mitatu pamoja na shindano ambalo lina lengo la kuwaongezea uwezo wajasiriamali wadogo kwa kuwapatia stadi za biashara, ufahamu na kisha kuwapatia zaidi ya Tsh. Milioni 10 kwa wazo bora la biashara litakalokuwa limewasilishwa.
Shindano hilo linalojulikana kama ‘Kuza Ofisi na FINCA’ kwa kuanzia litafanyika katika wilaya nne za mkoa wa Dar es salaam ambazo ni Kinondoni, Ilala, Temeke na Ubungo. Wilaya hizi zitaambatanishwa katika matawi ya benki yaliyoko Tegeta, Ilala, Victoria na kando ya barabara ya Pugu kuelekea uwanja wa ndege.
Akiongea wakati wa uzinduzi jijini Dar es salaam, Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa FINCA Nicholous John amesema lengo ni kuwapatia elimu ya biashara na fedha wamiliki wa biashara ndogo ndogo ambao baadae itapelekea katika kukuza biashara zao, Mshindi wa programu na shindano hili atawezeshwa kifedha kuendeleza biashara zake ndogo ndogo ziliyopo.
“Shindano hili litashirikisha wateja wa FINCA wenye akaunti na wale ambao wanapenda kushiriki watatakiwa kufungua akaunti ya FINCA, ambao pia watatakiwa kuweka kiasi cha Sh. 20,000 (Salio jipya katika akaunti zao) Watatakiwa kujaza fomu katika matawi ya FINCA ambapo watabainisha katika fomu hizo kuwa wataenda kufanyia nini zawadi hiyo katika biashara zao iwapo wataibuka kuwa washindi. Baada ya hapo fomu hizo zitawasilishwa katika matawi yetu, mpaka hapo watakuwa wametimiza vigezo vya hatua ya kwanza ya shindano”.
“Hatua ya pili, washindani 8 watachaguliwa na jopo la majaji kushiriki katika kipindi cha televisheni ambacho kitajulikana kama ‘Kuza Ofisi na FINCA’ kitakachokuwa kinarushwa kupitia TVE. Mwishoni mwa shindano, mshindi mmoja mwenye bahati ataondoka na zawadi nono ya zaidi ya Tsh. milioni 10”, Alisema Nicholous, akiongeza kwamba washiriki wengine wenye vigezo pia watakuwa na nafasi ya kujipatia mikopo kutoka benki hiyo.
Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Biashara wa FINCA, Emmanuel Mongella amesema kampeni hiyo ni njia mojawapo ya kusherekea miaka 20 ya uendeshaji wa shughuli za benki hiyo nchini na kuongeza kuwa, FINCA imekuwa maarufu kwa utoaji wa huduma bora.