Benki ya Standard Chartered imezindua huduma mpya inayowawezesha wateja wake kupata huduma hadi 70 kupitia simu za kisasa (smartphone) bila kufika katika tawi lolote la benki hiyo. Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Sanjay Rughani amesema wanategemea kupata wateja 40,000 hadi kufikia mwezi Desemba kutokana na kuanza kwa teknolojia hiyo iliyozinduliwa jijini Dar es salaam hapo jana.
“Tanzania imekuwa nchi ya tatu kuzindua mfumo huu miongoni mwa nchi 70 ambazo Standard Chartered tunatoa huduma, mfumo huu unarahisisha huduma kwa kuwa na gharama ndogo lakini pia kwa kuwa matumizi ya simu ni makubwa utasaidia kujumuisha watanzania wengi katika huduma za kifedha”. Amesema Rughani.
Hata hivyo Mkuu wa benki hiyo ukanda wa Afrika na Mashariki ya Kati, Jaydeep Gupta ameeleza kuwa hadi sasa wametumia takribani Dola za kimarekani Bilioni 1.5 kuendeleza teknolojia mbalimbali kwa kipindi cha miaka mitatu katika benki hiyo na wanaendelea kufanya uzinduzi katika nchi nyingine ili wateja wao waweze kufurahia huduma.