Mkurugenzi Mkuu wa benki ya KCB Cosmas Kimario amesema benki hiyo imetenga takribani Sh. 100 bilioni kwa ajili ya kukopesha makundi ya wajasiriamali wadogo kote nchini ili waweze kuendeleza biashara zao. Kimario amesema hayo wakati akifungua mafunzo ya wajasiriamali waliounganishwa na benki hiyo kwa lengo la kuwapa uwezo wa kuchangamkia fursa za kibiashara.
Kimario amedai kuwa, benki hiyo imesukumwa kutenga kiasi hicho kwa mwaka wa fedha 2018/19 ili kuwakopesha wajasiriamali na kuwasaidia kuinua vipato vyao. Benki hiyo pia imejipanga kuwafikia wakulima vijijini na kutoa mikopo itakayowasaidia kuendesha kilimo cha kisasa na chenye tija. Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa wameamua kufanya hivyo kutokana na wafanyabiashara wadogo wengi kukata tamaa kutokana na kukosa maono ya biashara.
Kwa upande wake, Mtaalamu wa masuala ya kodi Adolf Lyimo moja kati ya matatizo yanayowakumba wafanyabiashara wadogo ni kukosa elimu ya kutosha kuhusu kuhusisha biashara zao na masuala ya kodi ambapo wengi wamekuwa wakifanya biashara bila kujua namna sahihi ya kupangilia kodi na faida wanayotengeneza hivyo kushindwa kufikia malengo yao.