Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya NMB Ineke Bussemaker amewaambia waandishi wa habari kuwa benki hiyo imeanza kutoa mikopo ya hadi Sh. 150 milioni kwa wafanyakazi nchini ndani ya siku moja huku muda wa marejesho wa mikopo hiyo ukiongezeka na kufikia miaka sita. Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa mikopo hiyo itajumuisha wafanyakazi kutoka sekta binafsi na serikalini bila ubaguzi wowote na kwamba, kinachoangaliwa ni mikataba ya kudumu au ile ya muda mrefu.
Imeelezwa kuwa mfanyakazi anaweza kupatiwa mkopo wa hadi Sh.150 milioni ambao unaweza kulipwa kidogo kidogo kwa kipindi cha miaka sita. Vilevile, NMB imepunguza riba kwa wafanyakazi wote kutoka asilimia 19 mpaka 17.
Utoaji wa mikopo hiyo ni muendelezo wa sekta ya benki hapa nchini kutoa mikopo ya kima kilichoongezeka na masharti nafuu, huku riba za benki zikipungua kwa viwango tofauti tofauti.
Akiwa mjini Dodoma mwishoni mwaka jana, Rais Magufuli aliagiza benki kuangalia uwezekano wa kupunguza riba ya mkopo na baadhi ya benki kama CRDB, BOAT na NMB zimeonyesha kumuunga mkono na kufanya hivyo.