Benki ya NMB imeanza mazungumzo na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili kuona ni namna gani wanaweza kusaidia kilimo cha michikichi mkoani Kigoma ili wananchi wanaojishughulisha na kilimo hicho waweze kufaidika. Mkuu wa wateja wakubwa na serikali wa benki hiyo Filbert Mponzi ameweka wazi mpango huo alipozungumza na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati wa mkutano mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa jijini Dodoma.
Mponzi ameeleza kuwa kwa sasa, NMB inahudumia wakulima wadogo takribani milioni 15 nchi nzima na kueleza kuwa benki hiyo itaendelea kutenga fedha maalum kwa ajili ya wakulima wengi zaidi.
“Kwa sasa NMB imetenga zaidi ya Sh. 500 bilioni kwa ajili ya kusaidia wakulima hapa nchini lengo likiwa kusaidia jitihada za serikali ya awamu ya tano ya uchumi wa viwanda kupitia sekta ya kilimo”. Ameeleza Mponzi.
Wakiwa katika mazungumzo hayo, Majaliwa alisisitiza kuwa serikali imejipanga kuwekeza vya kutosha katika kukuza kilimo cha michikichi na kuitaka benki hiyo kuisaidia serikali katika harakati zake za kuwasaidia wakulima wa Kigoma.
“Tumekuwa tukiwashawishi wakulima mkoani Kigoma kujikita katika kilimo cha michikichi lakini kwa bahati mbaya wakulima wengi hawana mitaji ya kulima michikichi kwa wingi. Nitafurahi kama benki yenu kupitia mikakati yake itawezesha wakulima wa michikichi”.Alisema Majaliwa.