Serikali imepokea gawio la Sh. 10.17 bilioni kutoka Benki ya NMB. Fedha hizo ni sehemu ya jumla ya Sh. 32 bilioni zilizodhiinishwa katika mkutano mkuu wa mwaka wa wanahisa uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es salaam.
Akizungumza kabla ya kukabidhi mfano wa hundi ya fedha hizo kwa Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Philip Mpango, Mkurugenzi Mkuu wa NMB Ineke Bussemaker ameseam benki hiyo imedhamiria kuwezesha watanzania zaidi hasa wakulima kufikiwa na huduma za benki popote walipo.
Bussemaker ameeleza kuwa mbali na kutoa gawio hilo ambalo limetokana na taasisi hiyo ya kifedha kupata faida mwaka 2017, NMB imejipanga kuboresha huduma za jamii na kuhamasisha wakulima zaidi nchini kuanza kutumia mifumo rasmi ya kutunza fedha.
Kwa upande wake, Waziri Mpango ameishukuru benki hiyo kwa kufanya kazi kwa bidii na hata kupata faida japokuwa sekta ya fedha ilikumbwa na changamoto nyingi mwaka jana. Ameshauri kampuni nyingine ambazo serikali ni wanahisa kuiga mfano wa benki hiyo na kuanza kutoa gawio ambalo serikali itatumia kwa malengo yaliyokusudiwa.