Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Augustino Chacha amesema benki hiyo imeingia makubaliano na Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), makubaliano ambayo amedai yanalenga kuimarisha mnyororo wa thamani katika sekta hiyo hapa nchini. Akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano hayo jijini Dar es salaam, Chacha amesema kuwa lengo kuu ni kuinua na kuijenga upya sekta ya maziwa.
“Makubaliano haya yanalenga pia kuongeza tija na uzalishaji endelevu katika sekta ya maziwa nchini kwa kuwajengea uwezo wadau kwa njia ya elimu na teknolojia. Tumekubaliana kuwajengea uwezo wadau wa mnyororo wa thamani ya maziwa kwa njia ya mafunzo na kimtaji”. Amefafanua Chacha.
Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa TDB, Lucas Malunde amesema lengo kubwa ni kuanzia hatua ya uzalishaji, uchakataji na uuzaji wa bidhaa zilizopo kwenye mnyororo wa thamani wa maziwa. Malunde pia ametumia nafasi hiyo kuipongeza TADB kwa kutoa elimu ili kuwaongezea wadau tija.
“Bodi itashirikiana na TADB katika kutoa elimu na utaalamu ili kuongeza tija katika uzalishaji ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wa kutumia vizuri fursa za mikopo inayotolewa na benki”. Amesema Malunde.