Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) imeingia makubaliano na NMB pamoja na Benki ya Posta (TPB), makubaliano ambayo yanalenga kuwasaidia wakulima wadogo kupitia Mfuko wa Dhamana kwa Wakulima Wadogo ulio chini ya TADB. Makubaliano hayo yanadhamiria kumuwezesha mkulima mdogo kumudu kufanya kilimo chenye tija, kuondokana na umaskini na kufanikisha lengo la serikali la kufikia uchumi wa kati mwaka 2025.
Akizungumza baada ya kikao cha pamoja, Meneja wa Mfuko huo James Mwakilima amesema serikali tayari imeshatoa Sh. 45 bilioni ili mfuko huo uweze kutoa mikopo kwa wakulima wadogo kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini.
“Katika kutimiza azma yake ya kujenga uchumi wa kati na viwanda, serikali imeshatoa Sh. 45 bilioni kwa TADB kupitia Mfuko wake wa Dhamana kwa Wakulima Wadogo, ili wakulima waweze kujikita kwenye kilimo chenye tija”. Ameeleza Mwakilima.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Mikopo wa TPB, Ramadhan Mganga amesema benki hiyo imefanikiwa kukopesha wakulima wadogo kupitia Mfuko huo huku akitaja baadhi ya mikoa iliyonufaika kuwa ni Simiyu, Singida na Iringa.
“Kupitia Mfuko huu wa Dhamana kwa Wakulima Wadogo, Benki ya Posta imewakopesha wakulima zaidi ya Sh. 3.5 bilioni kwa kipindi cha miezi sita tu tangu tusaini makubaliano”. Amesema Kaimu huyo.