Benki ya NMB jijini Mbeya imetozwa faini ya Milioni 12 kupitia Mahakama ya hakimu mkazi jijini humo baada ya kukutwa na hatia katika makosa matatu waliyoshitakiwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini. NMB imekumbwa na mkasa huo baada ya kukutwa na makosa ya kumpa mkataba wa kazi mkandarasi Kalongo’s General Supply ambaye hajasajiliwa na CRB.
Makosa mengine yaiyobainishwa ni pamoja na kukaidi tahadhari iliyotolewa na CRB na kutotii agizo lililoitaka benki hiyo kutoendelea na kampuni hiyo kwa kuweka mifumo ya kuzuia na kuzima moto kwenye matawi ya benki hiyo yaliyopo nyanda za juu kusini.
Kutokana na kosa hilo mahakama imemtia hatiani Mkurugenzi Mtendaji wa Kalongo’s General Supply, Japhet Sanga kwa kuendesha shughuli za kampuni bila vibali vinavyothibitisha uhalali wa kampuni hiyo na hivyo kutakiwa kulipa faini ya Sh. 3 Milioni.
Akisoma hukumu ya kesi hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Michael Mteite amesema ushahidi uliotolewa na shahidi upande wa mashtaka, Yusuf Denyelela,mahakama imejiridhisha NMB na mkurugenzi wa Kampuni hiyo walitenda kosa. Benki ya NMB imepewa siku 30 kuhakikisha inalipa faini hiyo na endapo itashindwa, mahakama itaamuru meneja wake kupelekwa jela.