Utafiti unaonyesha kuwa tabia na utaratibu kwa watoto huimarishwa zaidi katika umri wa miaka 9, hivyo tabia na utaratibu huo humjenga mtoto kadri anavyoendelea kukua na kumfanya awe na mwenendo fulani katika maisha.
Katika upande wa fedha wazazi hushauriwa kuwapa watoto mafunzo mbalimbali tangu utotoni ili kuwawezesha kujimudu na kufanikiwa wanapokuwa wakubwa, ndiyo maana benki zikapata wazo la kuanzisha huduma hadi kwa watoto ili kuwasaidia wazazi.
Akaunti za akiba za watoto ni nini?
Ni akaunti ambazo zinaweza kufunguliwa katika benki nyingi za kawaida na vyama vya mikopo kwa niaba ya mtoto. Lazima zifunguliwe kwa pamoja, nikimaanisha lazima kuwe na jina la mtoto na mzazi au mlezi katika akaunti husika. Kadri mtoto anavyokua ndivyo na benki itaendelea kuhamisha fedha zake kwa mfano kutoka katika akaunti ya watoto kwenda kwenye akaunti ya vijana, wanafunzi na hadi katika akaunti ya akiba ya watu wazima. Pia huwa kunakuwa na mifumo mbalimbali ya elimu kuhusu fedha ili kuwasaidia watoto tangu wakiwa na umri mdogo.
Kama wewe ni mzazi unayefikiria kumfungulia akaunti ya akiba mtoto wako kuna umuhimu wa kutambua mambo yafuatayo kabla ya kuchukua hatua hiyo:
- Lazima ufungue akaunti na mtoto. Benki huhitaji mtu wa miaka 18 au zaidi ili kuweza kufungua akaunti ya akiba. Mzazi hulazimika kuingia kama mmiliki wa akaunti ili kudhibiti wa akaunti hiyo. Licha ya hivyo, mzazi huwa hana mamlaka ya fedha zinazotoka na kuingia katika akaunti hiyo.
- Wote kwa pamoja (mzazi/mlezi na mtoto) huwa na uwezo wa kufikia fedha (kuzitoa na kuweka) zilizopo katika akaunti kwani wote ni wamiliki. Benki nyingi hazihitaji mtu mzima kuwepo wakati mtoto anafanya miamala.
- Ni vyema kuuliza nini kitatokea pale mtoto atakapokuwa mtu mzima, kulingana na masharti ya akaunti, mtoto anaweza kuwa na vikwazo kuhusu jinsi ya kutumia akaunti hiyo hadi atakapokuwa na miaka 18. Hii huepusha matumizi mabaya ya fedha zilizowekwa katika akaunti hiyo.
- Zingatia ada za akaunti,huduma na viwango. Ni dhahiri utataka kuchagua akaunti yenye ada ndogo na yenye viwango vikubwa vya riba lakini kuna vigezo vingine ambavyo ni muhimu kuzingatia kwamfano elimu nzuri ya kifedha.
- Usifikiri mtoto wako bado ni mdogo kuwa na akaunti ya akiba. Ni vyema kuanza mapema ili kumfundisha mtoto maadili na kurahisisha mwenendo wake wa maisha. Hii humsaidia kuzoea hali ya umiliki mapema hivyo anakua na uelewa kuwa kwa kujituma zaidi anaweza kumiliki zaidi.