Baada ya Mbunge wa Mbinga, Sixtus Mapunda kumuomba Rais wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli kuwachukulia hatua watu ambao kwa namna moja au nyingine walichangia kufilisi benki ya Mbinga Community, Rais Magufuli ameagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuwatafuta na kuwafikisha mikononi mwa Sheria wale wote waliohusika katika tukio hilo.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo wakati akiweka jiwe la msingi kwenye mradi wa barabara ya Mbinga-Mbamba Bay ambao unagharimu takribani Sh. 134.712 bilioni na kuwataka viongozi mkoani Ruvuma kufanyia kazi suala hilo ili wahusika wakamatwe na kujibu mashtaka kwa mujibu wa Sheria.
“Nafahamu kwenye miaka ya nyuma kulikuwa na benki hapa, lakini niliambiwa walioimaliza ni watu wa hapa hapa. Wananchi walilima kahawa vizuri, mkaanzisha benki yenu, benki ikaisha hadi ikafilisika. Ninachojiuliza, hawa walioifilisi benki hii wako wapi? Je, vyombo vya ulinzi na usalama vimechukua hatua gani? Je, kuna ukaguzi gani umefanyika kwa hawa watu tuliowapa imani kubwa ya kuanzisha chombo hiki kilichokuwa kinawasaidia wakulima wakulima hadi kikawafia mikononi mwao? Ninawaomba viongozi wa hapa Mkuu wa Wilaya, wakuu wa vyombo vya Takukuru, Mkuu wa Polisi wa Wilaya, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Mkuu wa Mkoa, tuanze kushughulikia suala hili”. Ameeleza Rais Magufuli.