Benki ya CRDB Tanzania imezindua huduma tatu mpya kwa ajili ya kuwarahisishia wateja wao kupata huduma za kibenki kwa urahisi zaidi kupitia simu zao za kiganjani.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam, Meneja wa Huduma za Fedha kwa njia ya mtandao wa CRDB, Edith Metta ametaja huduma hizo kuwa ni Akaunti ya akiba, Akaunti ya kikundi na Akaunti ya malipo.
Metta amesema kuwa benki ya CRDB imeamua kuanzisha huduma hizo zitakazokuwa zikifanyika kupitia simu za mkononi ili kuondoa changamoto ambayo imekuwepo kwa baadhi ya vikundi vya fedha ikiwemo Vicoba na vikundi vya wajasiriamali kama vile upoteaji wa fedha au mwanakikundi kukimbia na fedha, na kuongeza kuwa huduma hiyo itafuta kabisa changamoto hizo.
Akielezea jinsi huduma hiyo itakavyokuwa ikifanya kazi Metta amesema kuwa wanakikundi wataweza kufungua akaunti itakayowawezesha kuweka pesa na kuitoa bila malipo yoyote.
“Mwanachama ana uwezo wa kuangalia salio katika akaunti ya kikundi na endapo kuna fedha imetolewa kinyemela, wanajua kwa wakati na kuepusha mwanachama kukimbia na fedha au kuambiwa fedha zimeibiwa” Alisema.
Metta amesema huduma hii inatarajia kuwa mkombozi kwa vikundi vya vicoba na vikundi vya ujasiriamali kwa sababu itaepusha udanganyifu na endapo kuna udanganyifu umefanyika miongoni mwa wana kikundi itakuwa rahisi kuchukua hatua za haraka za kumshughulikia.