Biashara baina ya Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) imetajwa kuwa ni kiasi kinachofikia Dola za Marekani bilioni 3.2.
UAE imetajwa kuwa mshirika namba saba kwenye eneo la biashara na uwekezaji Tanzania.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk amebainisha hayo katika kumbukizi ya miaka 52 ya Siku ya Taifa ya Umoja wa Falme za Kiarabu yaliyofanyika Novemba 22, 2023 Jijini Dar es Salaam na kuwasihi kuendelea kufanya biashara na kuwekeza kwa wingi nchini.
Balozi Mbarouk amepongeza juhudi za viongozi wa mataifa hayo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa UAE, Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan, kwa uongozi wao imara wenye maono na juhudi za kuimarisha na kudumisha uhusiano baina ya nchi hizi mbili.
Balozi Mbarouk amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeuhakikishia Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) mazingira salama ya biashara na uwekezaji nchini.
Amesema Serikali imefanya jitihada mbalimbali katika kuhakikisha kuwa mazingira ya biashara na uwekezaji yanaboreshwa ili kutoa fursa kwa wawekezaji wengi kuwekeza nchini.
“Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuweka sera imara, sheria na taratibu rafiki pamoja na kuweka misingi thabiti ya kustawisha mazingira ya biashara,” amesema Balozi Mbarouk.
Kwa Upande wake, Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu nchini, Khalifa Abdulrahman Al Marzouqi amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa uhusiano baina ya UAE na Tanzania mwaka 1974, nchi hizo zimejitahidi kuendeleza na kuimarisha uhusiano huo katika nyanja mbalimbali kwa maslahi ya pande zote mbili.