Mwenyekiti wa zamani wa Bodi ya Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) Captain Mstaafu John Chiligati ametoa wito kwa halmashauri hapa nchini kutenga maeneo maalum kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo wadogo ili kuwasaidia kuweza kupata mikopo kutoka taasisi mbalimbali za kifedha.
Chiligati ametoa ushauri huo alipokutana na uongozi wa wilaya na halmashauri ya Urambo na kuongeza kuwa, katika halmashauri mbalimbali, uongozi umekuwa ukitumia fedha nyingi kwa ajili ya kuwalipa mgambo ambao wamekuwa wakifukuza wafanyabiashara wadogo wadogo wanaoendesha biashara zao maeneo yasiyo rasmi badala ya kutumia fedha hizo kutengeneza miundombinu na mazingira rafiki kwa wajasiriamali hao kwa kutenga eneo moja ambalo wataendesha shughuli zao.
“Nawaomba halmashauri tengeni maeneo ambayo mtawapanga wafanyabiashara kulingana na shughuli zao,kama ni nguo mtaweka sehemu fulani kama anauza viatu atakuwa eneo lake ili kuwarahisishia watu wa benki kuwapa mkopo wajasiriamali kwa sababu benki haziwezi kukopesha mtu anayetembeza bidhaa”. Amesema Mstaafu huyo.