Kufuatia ajali iliyotokea jijini Dodoma na kuwajeruhi wafanyabiashara waliokuwa wamepanga biashara zao kandokando ya barabara, Ofisa Masoko wa jiji hilo James Yuna amewasisitiza wajasiriamali kuacha kupanga biashara zao maeneo yasiyo rasmi hususani kandokando ya barabara.
“Upangaji huo wa biashara usio rasmi umekiuka taratibu na mbaya zaidi wanahatarisha maisha yao na ya wateja pia”. Amesema Yuna.
Pia amewataka wajasiriamali hao kuhamishia biashara zao katika maeneo maalumu waliyotengewa huku akitaja baadhi ya maeneo rafiki kwa ajili ya kuendesha biashara kuwa ni pamoja na soko la Bonanza, soko kuu la Majengo, Sabasaba, Chang’ombe, pamoja na soko la jioni Nyerere Square.
Ofisa huyo amesema kuna umuhimu wa kutumia masoko hayo badala ya kufanya biashara zao mitaani na barabarani ili kuepuka na majanga ya ajali kwa watembea miguu na wateja wa biashara hizo. Aidha, amewataka wafanyabiashara jijini humo kuzingatia maelekezo sahihi wanayopewa na halmashauri ili biashara zao zilete tija kiuchumi.