Katibu wa Shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) wilayani Kahama, mkoani Shinyanga Robert Nghomano ametoa wito kwa serikali kuwapunguzia kodi watu wenye ulemavu ambao wanamiliki biashara ndogondogo ili kuwapa fursa ya kujikwamua kiuchumi na vilevile kuchangia katika uchumi wa taifa.
Nghomano amesema hayo katika semina ya elimu ya Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha kwa makundi maalum iliyoandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango na kuishauri serikali kuwaangalia wafanyabiashara walemavu huku akieleza kuwa, endapo kuna uwezekano, serikali itoe msamaha wa kodi hizo kwani walemavu wengi wamekuwa na mazingira magumu ya kufanya biashara kutokana na hali zao.
Naye Mchumi Mkuu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Dionisia Mjema amesema kuwa kodi ina umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya taifa, na kutaka Shirikisho hilo kuandika andiko rasmi na kuliwasilisha katika Wizara hiyo ili waweze kusaidiwa kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
“Sasa hivi Wizara inapokea mapendekezo ya misamaha ya kodi, kama mnahitaji msamaha andikeni andiko mueleze sababu za msamaha huo na serikali itapata nini katika msamaha huo, ili kamati iangalie na kujiridhisha mtapata”. Amesema Mjema.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, Katibu Tarafa wa Kahama, Julias Chagama ametoa wito kwa wafanyabiashara wadogo kujitokeza kwa wingi na kuchukua vitambulisho.