239
Ukiwa mwenye akili timamu ni lazima uwe na changamoto ya maisha na kila kukicha ni lazima ujue ni jinsi gani ya kuweza kufanya maisha yako yakaendelea bila kua tegemezi.Zifuatazo ni aina kumi ya biashara unazoweza kufanya bila kua na mtaji mkubwa….
1. KUPIKA KWA ODA
Kama wewe ni mpishi mzuri au una mtu anayejua kupika, basi jitangaze kama unapokea oda za mapishi fulani.
Tuchukulie unaweza kupika makande au wali nyama vizuri.
Unachoweza kufanya ni kwenda maofisi ya karibu yako na kuwaambia kwamba wakutafute wanapohitaji hicho chakula wakati wa mchana na wewe utawaletea.
Usisahau kuacha mawasiliano yako ili waweze kukutafuta.
Wengi wao watapenda hiyo huduma kwasababu hawatohitaji kutoka tena kufata chakula.
2. UREMBO (MAKEUP, KUSUKA & KUCHA)
Urembo ni gharama. Wanadada wanataka kupendeza wanapokwenda safari zao kama ni kazini ama shughulini.
Uzuri ni kwamba hii ni biashara ya kila siku unayoweza kufanya.
Baada ya kufanya utafiti wangu, nimebaini kwamba kufanya makeup, kutengeneza kucha na ususi wa nywele zinalipa vizuri tu.
Kuna watu wengi tu wanaendesha maisha yao kupitia biashara hizo. Kwanini wewe ushindwe? Na kama sio mtaalamu, hakuna tatizo.
Chukua muda wako na kujifunza, ndani ya muda utaweza.
3. KUUZA JUISI NA ICECREAM
Kujifunza kutengeneza juisi au icecream haitakuchukuwa muda mrefu. Ili kufanikiwa katika biashara hii, cha muhimu ni kujitofautisha.
Muhimu zaidi unapofanya biashara ya kutengeneza juisi au icecream, ni kuweka mazingira yako safi na salama kwa wateja wako.
Uzuri wa biashara hii ni kuwa mtaji wake ni mdogo sana.
Elfu kumi tu inatosha kuanzia na wapo waliofanya hivyo na wamekuza biashara zao.
4. KILIMO CHA MBOGAMBOGA
Kilimo ni sehemu kubwa ya maisha ya watanzania na wale wa nchi nyingi za Afrika.
Kila siku zikienda, kilimo huzidi kuwa ni biashara ya matajiri kwasababu shamba lina gharama kubwa.
Licha ya hivyo, bado kuna fursa ya kutengeneza kipato kupitia kilimo cha mbogamboga hata kama una mtaji mdogo.
Anza na sehemu ndogo tu unayoweza kupata hata kama ni nyumbani.
5. UFUGAJI WA KUKU, BATA, N.K)
Hii ni biashara ambayo ina faida kubwa lakini pia ina changamoto zake kama vile kuku wako kufa.
Vifo vya mifugo huwaumiza sana wafugaji na mara nyingi husababishwa na mifugo hiyo kula uchafu.
Hivyo, unapoingia kwenye ufugaji jitahidi uwe na mazingira safi na salama kwa mifugo yako.
Usafi wa mara kwa mara hasa hasa kwenye malisho yao utahitajika.
Kwa vile mtaji ni mdogo, unaweza kuanza na kuku wa kienyeji, bata au hata njiwa. Japo kuwa wanachukuwa muda ila kuwa mvumilivu, faida utaiona.
6. KUPIGA PICHA
Tangu kuja kwa mitandao ya jamii kama vile Instagram, watumiaji wa mitandao hiyo hutaka picha nzuri.
Hapo ndipo unapojitokeza wewe na kuwapa huduma yako ya kupiga picha.
Upigaji wa picha ni fani kama fani yengine, ili ujitofautishe pendelea kujifunza kwa wanaojua au tumia YouTube kujifunza.
Vifaa vya upigaji picha vina gharama ila sio lazima viwe vyako, muhimu ni kuwa na ujuzi. Vifaa unaweza kumuazima rafiki yako au kukodi.
7. KUTENGENEZA TOVUTI (WEBSITES)
Tuko katika ulimwengu wa habari na teknolojia, hivyo kampuni ama biashara ambayo hawako mtandaoni wanakosa wateja.
Ichangamkie fursa hiyo kwa kujifunza kutengeneza websites kupitia YouTube.
Kisha, tafuta biashara/ makampuni ambayo hawana tovuti na uwaelezee umuhimu wa kuwa na tovuti.
Mwisho, waambie kuwa wewe unatoa huduma hiyo.
Kwa kuanza, wateja wako wa mwanzo unaweza kuwafanyia kwa bei ya punguzo halafu mbeleni ukapandisha. Njia hii itakusaidia kupata mabalozi watakao kupatia wateja wengine.
8. KUPANGA SHEREHE/MATUKIO
Kuanzia maharusi, kitchen party, sendoff na sherehe nyenginezo nisizozifahamu. Zote hizi ni fursa ambapo unaenda kusaidia watu kuandaa sherehe zao mwanzo mpaka mwisho.
Wewe ndio unaumiza kichwa kutafuta watu na huduma mbalimbali kama vile wapambaji, ma dj, au kuwatafutia gari ya kukodi, kuwapikishia chakula na megine mengi.
Unachohitaji kuweza kufanya biashara hii ni uwe unawajua watu husika wanaotakiwa kwenye sherehe hizo.
Mfano, ujue wapambaji wa ukumbi, wapishi wa maharusi, ma dj ili uweze kuwapa kazi hizo. Utalipwa kwa kufanya kazi hiyo.
9. KUTEMBEZA WATALII
Hii nayo ni biashara nyengine ambayo haihitaji pesa kabisa.
Unachohitaji ni kufahamu historia ya nchi yako hasa hasa ile ya maeneo ambayo watalii wanapenda kwenda.
Mfano, Zanzibar mtembeza watalii anaweza kulipwa kuanzia elfu ishirini kwa safari moja. Kwa siku ukipata safari tano tu unaondoka na zaidi ya laki moja.
10. USHONAJI NGUO
Kama wewe ni mpenzi wa mitindo, unaweza tengeneza kipato kizuri kwa kuwashonea watu nguo.
Itakuchukuwa muda kujifunza kushona ila ni kazi moja nzuri. Unapata kuwa mbunifu katika kutengeneza mishono mbali mbali na mwisho wake kulipwa.
Kama huna cherehani nyumbani, unaweza kwenda kukodi na kufanyia kazi zako hadi utakapo nunua yako.