Home BIASHARA Changamkia maonyesho ya biashara

Changamkia maonyesho ya biashara

0 comment 145 views

Maonyesho ya biashara hapa nchini yanakuja na umuhimu mkubwa kwa wafanyabiashara japokuwa wengi bado wamekuwa wazito kushiriki kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo gharama kubwa za ushiriki. Ni kweli lazima mfanyabiashara aingie gharama ili kushiriki kikamilifu lakini maonyesho haya yana umuhimu mkubwa kwao pamoja na kwa jamii nzima. Kama mfanyabiashara mwenye malengo ya kuimarisha biashara yako ni muhimu kuwa mshiriki katika maonyesho haya.

Maonyesho haya ni fursa nzuri kwa mfanyabiashara kukutana na wanunuzi wake na kufanya nao mazungumzo. Kupitia maonyesho ya biashara, inakuwa rahisi kukutana na wateja wengi zaidi na hivyo kuweza kuzungumza nao kuhusiana na bidhaa au huduma unayotoa. Unapata nafasi ya kupata maoni yao moja kwa moja na hivyo kujua wanachofurahia na kile ambacho hawafurahii katika biashara yako. Inakuwa rahisi kwa mfanyabiashara kujua ni kipi anatakiwa kubadilisha au kuboresha ili kukidhi mahitaji ya soko lake.

Kupitia maonyesho ya biashara pia, mfanyabiashara anapata uhakika wa moja kwa moja kuwa bidhaa zake zinapata kuonekana. Tofauti na kufanya biashara katika eneo moja ambalo soko ni dogo na wateja ni wa kuhesabika, maonyesho haya yanatoa nafasi kwa wateja kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi kufahamu biashara yako na kujenga mahusiano ya kudumu. Maonyesho haya ni fursa nzuri kwa mfanyabiashara kujitangaza na kuonyesha jamii nzima ni nini anafanya.

Kushiriki katika maonyesho ya biashara kunasaidia wafanyabiashara kuelewa soko kwa undani zaidi huku wakiwatambua washindani wao. Kupata nafasi ya kuwa katika mazingira pamoja na watu wanaofanya biashara sawa ile ambayo unafanya kunasaidia kutafakari na kufanya uchambuzi ili kubaini mapungufu yako pamoja na uwezo alionao mshindani wako ili kujiweka katika nafasi nzuri zaidi sokoni pamoja na kuboresha biashara yako kwa ujumla.

Wafanyabiashara nao wanatakiwa kutumia fursa hii kuinua biashara zao na kupanua soko zaidi. Mbali na wengi tulivyozoea, kuna maonyeho mbalimbali ya kibiashra yanayofanyika na sio sabasaba pekee. Hivyo wafanyabiashara pamoja na jamii kwa ujumla wanatakiwa kujenga mazoea ya kufahamu matukio kama haya yanapotokea na kutumia fursa hizo kuinua zaidi biashara zao. Wafanyabiashara wadogo na wajasiriamali wasikate tamaa kutokana na gharama kubwa zinazotumika kushiriki maonyesho haya, kwa kuanza wanaweza kwenda kama wageni na kufanya tathmini, kuangalia mazingira na kujiwekea malengo kisha kurejea maonyesho yanayofuata na kushiriki kikamilifu.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter