Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Hamza Johari amesema Shirika la ndege la Fastjet limepoteza sifa ya kuendesha biashara nchini na hivyo limezuia ndege moja kutoka shirika hilo kuruka kufuatia matatizo ya mara kwa mara na kukosekana kwa Meneja Mwajibikaji wa shirika. Johari amesema hayo leo wakati wa mkutano na waandishi wa habari ambapo ameeleza kuwa, tayari TCAA imetoa notisi ya siku 28 kuanzia leo ya kusudio la kufuta leseni ya shirika hilo.
“Tumekuwa tukiwaandikia barua ya kuwataka watueleze kuhusu mwenendo wao wa biashara tangu Fastjet Plc wajiondoe lakini pia shirika limekuwa na madeni mbalimbali ambayo hayajalipwa. Tukiomba watupe mpango wao wa fedha na biashara kwa mujibu wa Sheria hawafanyi hivyo”. Amesema Mkuu huyo wa TCAA.
Johari amesema shirika hilo linadaiwa na watoa huduma mbalimbali wakiwemo TCAA ambayo inadai kiasi cha Sh. 1.4 bilioni, lakini pia limekosa Meneja Mwajibikaji ambaye ni mtaalamu wa masuala ya ndege anayepaswa kutoa majibu ya hali ya ndege.
“Kwa sasa Fastjet hawana ndege. Ndege yao tangu jana tumeizuia kuruka kwa kuwa imekuwa ikipata hitilafu mara kwa mara na hawana mtu ambaye anaweza kutoa taarifa kuhusu mwenendo wake jambo ambalo linahatarisha usalama endapo itaruka”. Ameeleza Johari.