Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewaagiza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu na Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda kutayarisha muswada wa kuunganisha Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Shirikia la Viwango Tanzania (TBS) na kuwasilisha bungeni ili Sheria zake zipitiwe upya.
Majaliwa amesema hayo wakati alipofanya kikao na wafanyabiashara wa kati na wadogo na kueleza kuwa, mamlaka hizo zikiunganishwa, zitaweza kuepuka na malalamiko mengi kutoka kwa wafanyabiashara ambao wamekuwa wakidai kuwepo kwa tozo nyingi na urasimu kati ya taasisi hizo, hali inayopelekea taifa kupoteza wafanyabiashara na vilevile wateja.
“Sheria za TBS na TFDA zote zinafanana, ni maneno tu mnacheza nayo huku ubora, sijui viwango, vikiwa na viwango lazima vitakuwa bora, urasimu tu ndio uliokithiri TBS na TFDA, mizigo inakuja bandarini inakaa miezi miwili mitatu mnajifanya mnapima, mnapima nini?” Amesema Waziri Mkuu na kuongeza:
“Kama mashine zenu mbovu kwa nini msiagize mashine nyingine nje, Mkemia mkuu yupo kwa nini msiende kupima huko, mnakaa na bidhaa za watu muda mrefu mpaka zinaoza ndio maana wakati mwingine TRA wanaruhusu mizigo itoke mnakuja baadae kusema bidhaa haina viwango. Mawaziri wa wizara zote kaeni na taasisi zenu mbadilike, kama mashine yenu inachukua miaka mitano kutoa majibu basi nunueni zenye ubora, nimesikia TBS wanapima mpaka stuli za kukalia, hivi stuli unapima nini?” Amehoji Waziri Majaliwa.