Home BIASHARA Tanzania inatumia Bilioni 19.5 kuagiza mchuzi wa zabibu

Tanzania inatumia Bilioni 19.5 kuagiza mchuzi wa zabibu

0 comment 98 views

Tanzania hutumia takribani shilingi Bilioni 19.5 kila mwaka kuagiza wastani wa lita milioni 10 za mchuzi wa zabibu nje ya nchi ili kukidhi mahitaji ya ndani.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amesema hayo Agosti 19, 2024 wakati akizindua kiwanda cha kusindika zabibu kilichopo Chinangali II, Wilaya ya Chamwino jijini Dodoma.

Amesema kiwanda hicho kinakwenda kusaidia usindikaji na uhifadhi wa zabibu hivyo kuzuia upotevu wa mavuno unaotokana na hapo awali kukosekana kwa miundombinu ya kuongezea thamani na uhifadhi.

Dkt. Mpango amesema kiwanda hicho kitasaidia kukabiliana na changamoto ya upotevu wa zabibu kipindi cha uvunaji na uhifadhi ambapo inakadiriwa kuwa kati ya tani 17,683,500 ya zabibu zinazozalishwa asilimia 40% ya zabibu hupotea kutokana na ukosefu wa miundombinu ya kuongeza thamani na uhifadhi na hivyo kusababisha hasara kwa wakulima na Serikali.
Kiwanda hicho ambacho kimegharimu kiasi cha Shilingi Billioni 2.1 kina uwezo wa kusindika tani 7 hadi 8 kwa siku ambapo ni sawa na kuhifadhi lita 1500 za mvinyo.


Kwa mwaka, kiwanda hicho kina uwezo wa kuchakata tani 300 na kuhifadhi lita 220,000 za mchuzi wa zabibu.

“Kiwanda hiki ni matokeo ya jitahada zenu za uzalishaji wa zabibu, sasa ili tuweze kunufaika na uzalishaji wa kiwanda hiki ninawaomba sana ndugu zangu wa Chamwino na mkoa wa Dodoma kwa ujumla ongezeni uzalishaji wa zabibu ambapo wengine mnaweza kuleta kwa ajili ya kusindikwa, wengine mkaleta mchuzi wa zabibu utakaokuwa na vigezo kwa ajili ya kununuliwa,” amesema Dkt. Mpango.

Ametoa hamasa kwa wananchi kuongeza uzalishaji wa zao la zabibu na mazao mengine ya kimkakati kwa kuwa ardhi ya Dodoma ni rafiki kwa kilimo. Ameongeza kuwa Serikali imejipanga katika upatikanaji wa masoko ya uhakika wa zao la zabibu kutokana na kuongezeka kwa wanywaji wa mvinyo.

Mbali na zao la zabibu, wananchi pia wamepewa hamasa ya kulima mazao mengine kama mitende, maembe au komamanga ili kukuza uchumi wa Dodoma na kuongeza mchango wa mkoa wa asilimia 3 katika Pato la Taifa.

Kuhusu uhitaji wa kuongeza uzalishaji katika zao hilo, Makamu wa Rais Dkt. Mpango amesema Mkoa wa Dodoma unazidi kukua ambapo ujenzi wa makazi nao kushika kasi na kupelekea maeneo ya kilimo cha zabibu kutokomea.

Hivyo, ameagiza Wizara ya Ardhi kupitia Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Deogratius Ndejembi kupitia mipango miji kuainisha na kutenga maeneo kwa ajili ya kilimo cha zabibu.

Aidha, Dkt. Mpango ameipongeza menejimenti ya Wizara ya Kilimo ikiongozwa na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe kwa hatua mbalimbali za upatikanaji wa masoko ya mazao ya kilimo, na kuelekeza Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) kufanya tafiti na kuzalisha miche bora ya mizabibu kwa ajili ya wakulima.

Makamu wa Rais Dkt Philip Mpango akiteta jambo na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe.

“Naipongeza Wizara kwa kusimamia utekelezaji wa mradi huu unaolenga kukabiliana na upotevu wa zao hilo katika shughuli nzima za uzalishaji,” amesema Dkt. Mpango.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter