Mabadiliko ya ukataji tiketi za huduma za usafiri kutoka za kawaida kwenda za mtandao (tiketi za kieletroniki) yameanza leo Januari 06, 2021.
Mabadiliko hayo yanaanza katika njia 15 za kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya Lindi, Mtwara, Tanga, Iringa, Ruvuma, Njombe, Mbeya, Tunduma,Rukwa, Kilombero, Morogoro, Malinyi, Ifakara na Mahenge yametolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra).
Taarifa ya Latra inasema kuwa tafiti zilizofanywa mara kwa mara zinaonyesha kuwa wasafirishaji wanapoteza zaidi ya asilimia 30 ya mapato yao ambayo inapotelea mikononi mwa watu wengine ambao sio wawekezaji katika sekta hiyo.
Tiketi mtandao ni programu ya kielektroniki kwa ajili ya ukataji wa tiketi za mabasi ambayo inamruhusu msafiri kupata tiketi bila ulazima wa kwenda kwenye ofisi za mabasi ambapo abira atakata tiketi yake kwa njia ya mtandao kupitia simu janja ama kupitia tovuti.
Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Gilliard Ngewe alisema baadhi ya kampuni za mabasi zimeomba kuongezewa siku saba.
Alisema “Mpango uliopo ni mabasi ya wilayani na daladala nayo kutumia tiketi mtandao. Asiyetumia mashine ya kielektroniki kukatisha tiketi njiani atapigwa faini na TRA Sh3 milioni na Latra ni Sh250,000.”