Zanzibar ni moja kati ya visiwa maarufu kabisa hapa Afrika. Kwa mujibu wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, wageni zaidi ya 300,000 hutembelea visiwa hivyo kila mwaka. Watalii hupendelea vivutio mbalimbali vilivyopo kisiwani humo. Kwa kiasi kikubwa uchumi wa Zanzibar unategemea sana tabia nchi kwani shughuli za utalii huangalia kwa kiasi kikubwa hali ya hewa. Uchumi wa visiwa hivi pamoja na maisha ya wananchi wake kwa ujumla hutegemea sana hali ya hewa kwani wamezungukwa na maji.
Watalii wengi hupenda kutembelea visiwa hivyo kujionea vivutio kama fukwe mbalimbali za bahari pamoja na maeneo mengine ya kihistoria. Sekta ya utalii ndiyo chanzo kikubwa cha mapato kwa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar lakini miaka ya hivi karibuni baadhi ya wananchi wamekuwa wakiendesha shughuli hatarishi ufukweni mwa bahari hali ambayo inatishia kasi ya utalii mahali hapo.
Fukwe ni miongoni mwa vivutio vinavyopendwa zaidi na wageni wanaotembelea Zanzibar lakini ni jambo la kusikitisha kuona baadhi ya wananchi wanaoishi karibu na bahari wakizitumia vibaya fukwe hizo kwa kuzifanyia uharibifu na kusababisha fukwe zile kuharibika na kupoteza ubora wake, hali ambayo kama ikiendelea inaweza kuathiri sekta nzima ya utalii ambayo mbali na kuingizia serikali mapato, pia ni chanzo kikubwa cha ajira kwa wazanzibari walio wengi.
Baada ya serikali kutoa agizo la kuwataka wananchi kuacha shughuli za uchimbaji mchanga ndipo changamoto hii ilipoanza kujitokeza kwani wananchi hao walianza kufanya shughuli hizo katika fukwe za bahari. Kuendelea kwa shughuli hizi mbali na kuondoa haiba pia kunaweka dosari katika upatikanaji wa mapato kupitia utalii kwani hakuna mtalii atakayefurahishwa na kuitangaza vizuri Zanzibar huko nje ikiwa wananchi wake wanaendelea kuharibu vivutio hivyo na kuikosesha serikali mapato.
Serikali kuanzia ngazi ya chini kabisa wanapaswa kuwaelimisha wananchi juu ya madhara makubwa ambayo shughuli hizi za uchimbaji zinaweza kuleta visiwani hapo. Pia wanayo nafasi kubwa ya kuzisimamia na kuzifanyia ulinzi kwa umakini mkubwa fukwe ili kuzinusuru na uharibifu huo unaoendelea. Vilevile, sheria kali ziwekwe ili kuwaadhibu wale wote watakaokamatwa kwa makosa haya.