Kuendesha biashara pekee ni jambo linalotumia muda mwingi hivyo unapoongeza vipengele vingine vya maisha ni rahisi kuona kuwa muda hautoshi kufanya kila kitu. Ukweli ni kwamba kuwa na ujuzi wa jinsi ya kusimamia muda wako na kazi ulizonazo husaidia mambo yako kwenda vizuri.
Ikiwa uko katikati ya masomo na unafanya biashara basi tumia vidokezo vifuatavyo ili kuhakikisha unapangilia muda wako vizuri.
1. Ratiba
Kuwa na ratiba kutaleta mafanikio katika masomo na kazi zako. Hivyo jitahidi kutenga muda wa masomo na biashara yako. Kila mwanzo wa wiki weka mipango ya jinsi siku yako itakavyokwenda ikiwa ni pamoja na kuweka alama katika kalenda yako katika siku ambazo utakuwa na mitihani. Hii itakurahisisha kupanga mipango kuhusu biashara yako. Jitahidi kuamka mapema kidogo au fanya kazi zako za darasani muda wa kula (mchana au usiku) ikiwa unapenda kulala muda mrefu zaidi.
2. Bajeti
Kwa kusoma huku unafanya kazi itakubidi upunguze baadhi ya michakato ambayo mwisho wa siku itapunguza kiwango chako cha mapato mwishoni mwa mwezi. Baada ya kuvunjika moyo na kuhangaika kuhusu fedha jitahidi kubadilisha mwenendo wa bajeti yako, na muda kama ipasavyo ili kurahisisha maisha yako mapya.
3. Afya ni muhimu
Unatakiwa kujua kuwa mwili wako utahitaji msaada wote unaoweza kupata ili kufanya kazi zote kwa ustahiki. Hivyo ni muhimu kula chakula ambacho ni rafiki kwa afya yako ili kuhakikisha afya yako iko salama na akili yako iko makini zaidi. Akili ikiwa makini itakuwa rahisi kukujifunza na kuzingatia mambo yanayohusu kazi na masomo.
4. Tenga muda wa kupumzika
Baada ya siku ndefu ya kujihusisha na maswala ya kazi na masomo unatakiwa kujiwekea muda wa kupumzika ili uweze kutafakari. Unaweza kupumzika kwa kusoma kitabu, kufanya vitu unavyofurahia kufanya, kuangalia televisheni n.k. Muda wako wa kupumzika unaweza kuwa jioni baada ya majukumu au asubuhi kabla ya majukumu.
Kumbuka hata kama unajiamini kuwa unaweza kufanya kila kitu, sio vibaya kusema hapana katika baadhi ya mambo kwani kuelemewa na kazi kutakwamisha michakato yako. Tambua mapungufu pamoja na mipaka yako na kumbuka kufanya vitu kulingana na uwezo wako. Sio vibaya kuwapa watu wengine baadhi ya majukumu yaliyopo.