Home BIASHARAUWEKEZAJI Kuifungua Kusini kiutalii ni kazi endelevu: CP. Wakulyamba

Kuifungua Kusini kiutalii ni kazi endelevu: CP. Wakulyamba

0 comment 18 views

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea na jitihada za kuifungua Kusini kiutalii kwa kuboresha usimamizi wa Maliasili na kukuza Utalii kwenye vivutio hivyo adhimu na adimu duniani hali itakayoongeza kuvutia watalii zaidi na kuchangia pato la taifa.

Hayo yamebainishwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia Maliasili, Kamishna wa Polisi (CP) Benedict Wakulyamba, alipokuwa akifungua kikao cha tisa (9) cha Kamati ya Uongozi ya Mradi wa REGROW, Mkoani Morogoro, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo.

CP. Wakulyamba amesema kuwa, kazi kubwa inayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwainua wananchi na Taifa kiuchumi kupitia sekta ya utalii hususan kupitia vivutio vilivyopo kusini mwa Tanzania ni ya kupongezwa na kuungwa mkono.

Ameongeza kuwa mradi wa REGROW hadi sasa umeonesha matokeo makubwa na chanya ambayo yanahitaji kuendelezwa ikiwemo ongezeko kubwa la watalii ukanda wa Kusini mwa Tanzania hasa katika Hifadhi za Nyerere, Mikumi, Ruaha na Udzungwa kwa watalii 135,000 mwaka 2024 ikilinganishwa na watalii 98,504 mwaka 2019 kabala ya mradi ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 100.

“Kupitia mradi huu mkubwa ulinzi na usalama katika Hifadhi zetu hizo umeongezeka sana pia zaidi ya wananchi 21,900 wanajipatia kipato mbadala kupitia shughuli za uzalishaji mali, COCOBA, pamoja na miradi ya vikundi. Haya nifanikio makubwa ”. Alisema CP. Wakulyamba.

Aidha CP. Wakulyamba amefafanua kuwa ni dhamira ya Serikali kuwaletea maendeleo wananchi wake, na kuwa ipo mikakati kabambe ya kuhakikisha kusini inainuka zaidi kiutalii hivyo inaendelea kukamilisha utekelezaji wa sehemu ndogo iliyobaki ya utekelezaji wa Mradi wa REGROW.

CP. Wakulyamba aliwapongeza wajumbe wa Kamati hiyo kwa kazi kubwa waliyoifanya katika utekelezaji wa mradi wa REGROW kwa kuwa ni chombo cha juu na jukwaa la maamuzi katika kuelekeza, kuongoza na kutoa maamuzi katika utekelezaji wa mradi huo wenye mchango mkubwa kwa maendeleo ya Jamii.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter