Home BIASHARAUWEKEZAJI Serikali ya Tanzania inaendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji, kodi: Mwigulu

Serikali ya Tanzania inaendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji, kodi: Mwigulu

0 comment 93 views

Waziri wa Fedha Dkt.Mwigulu Nchemba ameihakikishia Jumuiya ya Kimataifa na Watanzania kwa ujumla kwamba Serikali inaendelea kuweka na kuboresha mazingira ya uwekezaji ikiwemo kuboresha mifumo yake ya kodi.

Dkt. Nchemba ameyasema hayo Agosti 20, 2024 katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, Jijini Dar es Salaam, wakati akiagana na Balozi wa Uswisi aliyemaliza muda wake wa ubalozi hapa nchini, Didier Chassot.

Amesema kuwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ameunda timu ya wataalam ya kupitia na kuja na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha mifumo yake ya kodi ili kuvutia zaidi biashara na uwekezaji nchini.

Dkt. Nchemba amefafanua kuwa pamoja na kuundwa kwa timu hiyo, Serikali pia imechukua hatua kadhaa za kuboresha mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji kodi inayosaidia kukusanya mapato yake kwa ufanisi na kuondoa usumbufu kwa walipa kodi.

Ameelea kuwa lengo la kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji pamoja na kuimarisha mifumo ya kodi ni kuhakikisha kuwa idadi ya walipakodi inaongezeka hatua itakayosaidia pia kuiwezesha Serikali kupunguza viwango vya kodi ya ongezeko la thamani siku za usoni kwa sababi walipakodi watakuwa wengi.

Kwa upande wake Balozi wa Uswisi aliyemaliza muda wake hapa nchini, Didier Chassot ameipongeza Serikali kwa uamuzi huo wa kupitia mifumo ya kodi na kwamba anaamini Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini watapata pia nafasi ya kuzungumza na kujadiliana na Serikali kuhusu masuala hayo kama walivyoomba.

Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba akiwa na Balozi wa Uswisi aliyemaliza muda wake Didier Chassot.

Balozi Chassot alitumia fursa hiyo ya kuagana na Waziri Dkt. Nchemba na kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa hatua kubwa iliyopiga kimaendeleo katika kipindi kifupi.

Ameahidi kuwa Uswisi inaandaa mpango mpya wa ushirikiano wa kimaendeleo na Tanzania, utakaojielekeza katika kufanikisha agenda mbalimbali za maendeleo ya nchi kupitia program zake mbalimbali ikiwemo kusaidia mfuko wa maendeleo ya jamii-TASAF, usimamizi wa fedha za umma, biashara na uwekezaji kupitia asasi za kiraia na sekta binafsi.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter