Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewaomba wafanyabiashara wa Korea Kusini kuchangamkia fursa zilizopo kwenye sekta za viwanda na fukwe na kuwekeza. Waziri Mkuu ameyasema hayo alipokuwa akifungua jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Korea Kusini lililofanyika jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu Lee.
Majaliwa ameeleza kuwa Tanzania ni moja ya nchi zenye vivutio vingi na vikubwa ,ikiwa ni pamoja na hifadhi za taifa, Mlima Kilimanjaro, fukwe za bahari ya hindi, Ziwa Victoria na Tanganyika. Waziri Mkuu amesema Tanzania imekuwa ikifanya vizuri katika sekta ya utalii na uwekezaji kutokana na uwepo wa amani na utulivu.
Kwa upande wake, Waziri Lee ameishukuru serikali ya Tanzania kwa kuonyesha ushirikiano na Korea Kusini na kudai kuwa, ushirikiano huo unaendelea kudumishwa ili uwe wenye tija kwa mataifa hayo mawili. Ameongeza kwa kusema kuwa, Korea Kusini tayari inashirikiana na Tanzania katika nyanja za afya, elimu, sayansi na miundombinu.