Home BIASHARAUWEKEZAJI Uwindaji wa kitalii kuiingizia Tanzania bilioni 2.5 kwa mwaka

Uwindaji wa kitalii kuiingizia Tanzania bilioni 2.5 kwa mwaka

0 comment 12 views

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatarajia kuingiza jumla ya Dola za Kimarekani 968,000 sawa na shilingi za Kitanzania bilioni 2.5 kama ada ya vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa mwaka pamoja na mapato mengine.

Hayo yamesemwa Februari 21, 2025 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dkt. Pindi Chana wakati wa hafla ya kukabidhi vyeti vya umiliki wa Vitalu vya Uwindaji wa Kitalii kwa wawekezaji wanne (4), iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

“Ninayo furaha kukabidhi vyeti hivi kwa wawekezaji ambao ni K&F Wild Expedition Ltd kwa Kilwa Open Area Nakiu, Michel Mantheakis Safaris Ltd kwa Muhesi GR, Out of Africa Ltd kwa Lwafi Nkamba, Royal Conservation Ltd kwa Pori la Akiba la Pololeti na Selous MT2 kwa Neon Investment Ltd chini ya Uwekezaji Mahiri kwenye Maeneo ya Wanyamapori (Special Wildlife Investment Concession Areas-SWICA),” amesisitiza Chana.

Amefafanua kuwa utoaji wa vyeti hivyo kwa wawekezaji hao wapya unaendana na utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kutokana na ukweli kwamba hiyo inahalalisha umuhimu wa tasnia ya uwindaji kwa uchumi wa nchi na kusisitiza kuwa Utalii wa Uwindaji huchangia manufaa ya moja kwa moja kwa jamii kupitia ajira na maendeleo ya jamii.

Chana ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wengine kutoka China na duniani kuwekeza katika Sekta ya Utalii nchini Tanzania huku akimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mpango wa kuitangaza Tanzania katika kiwango cha kimataifa kupitia filamu za “Amazing Tanzania” na “Tanzania, The Royal Tour”.

“Napenda kuwahakikishia wadau wote wa uwindaji kwamba dhamira ya Serikali ni kuendelea kuweka na kudumisha mazingira wezeshi ya biashara zao bila kuathiri uhifadhi na ustawi wa watu wetu,” amesema Waziri Balozi Chana.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya TAWA, Meja Jenerali Mstaafu Hamis Rajabu Semfuko alisema kuwa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania  (TAWA) imekuwa ikitumia mikakati ya kimasoko kuvutia wawekezaji kutoka duniani kote ikiwa ni pamoja na matumizi ya mnada wa kielektroniki wa vitalu vya uwindaji ambapo kwa mara ya kwanza imefanikiwa kupata wawekezaji kutoka China katika sekta ya uwindaji.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter