Home BIASHARA Vibali kuagiza sukari nje ya nchi mwisho mwaka huu

Vibali kuagiza sukari nje ya nchi mwisho mwaka huu

0 comment 184 views
Serikali imesema haitatoa vibali vya kuagiza sukari nje ya nchi ifikapo 2022 hivyo makampuni ya kuzalisha sukari yanatakiwa kuongeza kasi ya uchakataji wa miwa ya wakulima na kuzalisha sukari ya kutosha mahitaji ya ndani.
Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda amesema “mwaka huu vibali vya kuagiza sukari itakayopungua vitatolewa kwa utaratibu wa kawaida, lakini ifikapo mwaka 2022 hakutakuwa na vibali vya viwanda na ikilazimu basi Bodi ya sukari ndio itapewa kibali cha kuagiza sukari itakayopungua”.

Prof. Mkenda alisema serikali inafuatilia kwa karibu utendaji kazi wa viwanda vya kuchakata sukari nchini kuona kama vinaweka mikakati ya kuongeza uzalishaji wa sukari kwa kushirikiana na wakulima wa miwa kwa kuwa mpango wa serikali ifikapo 2022 ni kuacha kuagiza bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi.

Alisema “tatizo letu la upungufu wa sukari halitokani na kukosa miwa, bali ni uwezo mdogo wa viwanda vya kuchakata miwa yote ya wakulima mchini hali inayosababisha baadhi ya miwa ya wakulima wetu kukosa soko”.

Katibu Tawala wa mkoa wa Morogoro, Mhandisi Emanuel Kalobelo alisema mkoa huo una viwanda vitatu ambavyo bado uzalishaji wake n mdogo.

Alivitaja viwanda hivyo na uzalishaji wake kuwa ni Kilombero Sugar Ltd I na Kilombero Sugar II ambapo kwa pamoja huzalisha tani 126,000 na kiwanda cha Mtibwa tani 50,000, huku uzalishaji wa miwa kwenye bonde la Kilombero unaofanywa na wakulima wadogo ukiwa umefikia wastani wa tani 800,000 hadi 1,000,000 na uwezo wa kiwanda cha Kilombero ni kuchakat tani 600,000 tu za wakulima hao kwa mwaka.

Takwimu za Bodi ya Sukari Tanzania  zinaonyesha kuwa uzalishaji kwa mwaka ni takribani tani 300,000 ambapo kwa mwaka 2020/2021 ulifikia tani 377,527 huku mahitaji kwa matumizi ya kawaida na viwandani ni tani 655,000.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter