Na Mwandishi wetu
Mwanaharakati wa masuala ya elimu, uchumi wa wakina mama na afya bora kwa watoto Africa Bi Graca Machel amehimiza vijana kutoka nchi za kiafrika kuacha malalamiko yasiyo na tija na badala yake kujiunga kwa pamoja na kutumia sauti yao kuonyesha serikali changamoto mbalilmbali wanazokumbana nazo kiuchumi na kijamii.
Ameyasema hayo jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza na vijana kutoka pande tofauti za Afrika kujadili changamoto zinazowakabili. Bi Machel ameongeza kuwa ni kweli serikali hazifanyi jitihada za kutosha kusaidia vijana kupata maendeleo lakini vijana wakilalamika tu bila kuchukua hatua stahiki hakuna kitakachobadilika.
Nchi za kiafrika zinashauriwa kuwekezakatika ubunifu walionao vijana wao. Kadhalika badala ya kutegemea serikali kutatua matatizo yao yote, vijana wanapaswa kutazama sekta nyingine kama kilimo ili kupambana na tatizo la ajira ambalo limekuwa la muda mrefu barani hapa.
Serikali nazo ziangalie upya mifumo ya elimu katika nchi zao kwani ni wakati wa mabadiliko. Afrika haiwezi kuwa na maendeleo kama hatuna mifumo itakayochochea mabadiliko kwa vijana wake. Kwa pamoja wananchi na serikali zao zishauriane matatizo mbalimbali yaliyopo kwa kufanya hivyo basi, watapata njia sahihi ya kuyatatua matatizo hayo.
Graca Machel ambae alikuwa mke wa kwanza wa Nelson Mandela ni mwanaharakati anayefahamika duniani kote kwa kazi zake za kutetea haki za wanawake na watoto. Amekuwa mstari wa mbele katika masuala ya uongozi bora,wanawake na shughuli za kimaendeleo, elimu na afya bora barani Afrika kwa muda mrefu sasa.