Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Bilinith Mahenge amezindua duka na ofisi za kampuni ya Vodacom Plc jana mkoani humo. Duka hilo linategemewa kutoa huduma katika mkoa huo na mkoa wa Singida.
Wakati wa uzinduzi huo Mkuu wa mkoa huyo, ameiagiza Kampuni hiyo ya simu kuboresha mawasiliano ili kukabiliana na changamoto ya mtandao huo kukatika katika baadhi ya maeneo mkoani humo.
“wekezeni katika katika mawasiliano wakati mwingine mtandao umekuwa unakatika, huduma sio nzuri katika baadhi ya maeneo” amesema.
Pia Mbunge wa Dodoma Mjini, ambaye ni Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde ameeleza kuwa kampuni hiyo imechangia katika mafanikio ya mpango wake wa kugawa kompyuta katika shule zilizopo jimboni kwake.
Naye, Mkurugenzi wa Uhusiano na Mawasiliano wa Kampuni hiyo, Rosalynn Mworia, amesema Kampuni hiyo ina minara zaidi ya 50 inayotoa huduma ya 4G na wana mpango wa kuongeza saiti nyingine 10 ili kuwezesha wananchi katika mkoa huo kunufaika na huduma za mawasiliano ya kidigitari na kwa ukaribu zaidi.
“Tumeona umuhimu wa kuongeza nguvu Dodoma kwa kufungua ofisi zetu na pia kuongeza duka jipya nia yetu ikiwa kuchochea shughuli za kiuchumi za mkoa huu” amesema Mkurugenzi huyo.