Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka wakuu wa Mikoa kuwapanga wamachinga katika maeneo stahiki bila kusababisha vurugu.
Akizungumza Septemba 13 Ikulu ya Chamwino, Dodoma wakati wa kuwaapisha viongozi aliowateua, Rais Samia amesema licha ya serikali kutoa fursa kufanya biashara kama njia ya ajira kwao, wamekuwa wakifanya kazi katika maeneo tofauti na wakati mwingine kuziba maduka ya watu.
“Watu hawa sasa wameenea kila mahali, hadi kwenye maduka wanaziba, wenye maduka hawauzi wanauza wao mbele hadi wenye maduka baadhi yao wamepata mtindo wa kutoa bidhaa ndani na kuwapa machinga kuwauzia kwa sababu watu hawangii ndani,” amesema Samia.
“Wito wangu pia kwa ndugu zetu wamachinga na wajasiramali, wajitahidi kufuata sheria na kanuni zilizopo, wajitahidi pia kufuata yale wanayopangiwa na wakuu wa Mikoa na wakuu wa Wilaya,” amesema Rais Samia.
Ameeleza kuwa kitendo hicho kinaikosesha serikali kodi kwa sababu wafanyabiashara hao hawalipi lakini mwenye duka anatakiwa kulipa kodi.
Soma: Biashara barabara za watembea kwa miguu marufuku: RC Makalla