Home FEDHABIMA Tsh. bilioni 117 zatolewa fidia kwa wakulima zao la tumbaku

Tsh. bilioni 117 zatolewa fidia kwa wakulima zao la tumbaku

0 comment 47 views

Shilingi Bilioni 117 zimetolewa katika benki ya NMB ikiwa ni fidia kwa wakulima wa zao la Tumbaku Mkoa wa Tabora.

Akikabidhi hundi hiyo kwa wakulima akiwa Makao Makuu ya Benki ya NMB, jijini Dar es Salaam Novemba 13, 2024 Waziri wa Kilimo Hussein Bashe ameipongeza Benki hiyo kwa kuendelea kushirikiana na wakulima nchini katika kuinua Sekta ya Kilimo, hususan kujenga mfumo wa bima kwa kila zao kutokana na viatarishi vyake.

“Takribani wakulima 2,226 kutoka AMCOS 22 watakwenda kupata fidia baada ya kupata changamoto ya mvua iliyoambatana na mawe na kuathiri zao la Tumbaku kwenye msimu wa killimo kwa mwaka 2023/2024,” ameeleza Waziri Bashe.

Ameongeza kuwa Benki ya NMB kwa kushirikiana na UAP Insurance wameendelea kufanya kazi nzuri kwa wakulima nchini katika kuhakikisha wakulima wanaendelea na shughuli za kilimo cha uhakika bila wasiwasi. Fidia inayotolewa kwa wakulima hao itaendelea kuwafanya wakulima kuwa na imani ya kujiunga na bima za kilimo.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaiguna amesema kuwa kwa msimu huu wa kilimo mwaka 2024/2025 Benki ya NMB imetenga zaidi ya kiasi cha Shilingi Bilioni 290 kwa wakulima wa zao la tumbaku nchini na kuwasihi wakulima kuendelea kushirikiana na benki hiyo ili kujipatia mikopo yenye riba nafuu inayomuwezesha mkulima kuendelea na kilimo cha uhakika kupitia bima ya kilimo.

Aidha, Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania, Baghayo Sakware ameeleza kuwa Selikali ina mpango wa skimu ya bima ya kilimo pamoja na kanuni za bima ya kilimo ili kuweza kusimamia kikamilifu masuala ya bima kwa upande wa kilimo nchini.

Nelson Rwihula ambae ni mwakilishi wa UAP Insurance amewasihi wakulima nchini kujiunga na bima ya kilimo itakayowasaidia kupata fidia pindi wanapopata majanga ya kimazingira kama mvua na mafuriko.

Akizungumza kwa niaba ya wakulima wa Usaguzi AMCOS, Ally Mrisho ameishukuru Benki ya NMB kupitia bima na kuahidi kuendeleza mshikamano ili kukuza Sekta ya Kilimo nchini.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter