Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, amewahimiza wamiliki na waendeshaji wa hoteli za kitalii nchini kuanza kutoa huduma ya kubadilisha fedha za kigeni ili kupunguza ubadilishaji holela wa fedha hizo.
Tutuba amesema hayo katika mkutano na wamiliki pamoja na waendeshaji wa hoteli zinazopokea watalii nchini uliofanyika katika ofisi za Makao Makuu Ndogo ya Benki Kuu jijini Dar es Salaam Machi 14, 2024.
Msingi wa kikao hicho kilichohudhuriwa na wamiliki 27 wa hoteli za kitalii unatokana na hatua iliyochukuliwa na BoT kurekebisha kanuni ya maduka ya kubadilishia fedha za kigeni.
Kanuni hiyo inaziruhusu hoteli za kitalii kupata leseni ya kutoa huduma ya kubadilisha fedha za kigeni kwa wateja wao.
“Mtakumbuka kwamba Oktoba 2023 tulitoa marekebisho ya Kanuni ya Maduka ya Kubadilisha Fedha za Kigeni ambapo tulitengeneza dirisha rasmi la kuruhusu hoteli kuanzia nyota tatu hadi tano kuanza kutoa huduma za maduka ya kubadilisha fedha za kigeni,” amesema Gavana Tutuba.
Aidha, Gavana Tutuba ameongeza kuwa maamuzi ya kufanya marekebisho ya kanuni hiyo yalitokana na utafiti uliofanywa na kugundua kuwa urasimishaji wa maduka ya fedha za kigeni haukugusa hoteli na hivyo kuongeza ubadilishwaji holela wa fedha za kigeni.
“Marekebisho ya kanuni ile yalitokana na utafiti tuliofanya ambapo tuligundua maduka ya kubadilisha fedha za kigeni yaliyokuwa yakiendeshwa yalikuwa bado hayajagusa hoteli lakini tukakuta hoteli nyingi zinapokea wateja wanaolipa fedha za kigeni lakini katika fedha zile nyingine zilikuwa zinabadilishwa kiholela,” ameeleza.
Gavana Tutuba amesema kuwa hatua hiyo itaisaidia BoT kupata takwimu na taarifa muhimu ambazo zitasaidia kuimarisha sekta ya fedha.
“Sisi kama wasimamizi wa sekta ya fedha, hatua hii itakuwa ni fursa ambayo itatufanya tuwe tunapata takwimu za moja kwa moja kwa sababu mtawajibika (hoteli) kuweka ule mfumo wa kupata taarifa ambao utatusaidia kuboresha mazingira ya biashara nchini,” amesema.