Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amezitaka taasisi zinazowezesha wananchi kifedha chini ya wizara hiyo kutowakopesha wajasiriamali ambao hawana namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN) kwa madai kuwa hawachangii katika pato la taifa ambalo linawezesha mikopo hiyo. Mwijage amesema hayo katika ufunguzi wa maadhimisho ya tamasha la kitaifa la wanawake wajasiriamali katika viwanja vya Nyerere Square mjini Dodoma.
“Msajili kwanza biashara zenu ili serikali iwatambue kuwa ni walipakodi na kodi ni kwa ajili ya maendeleo ya nchi. Haiwezekani unaomba fedha za mkopo, serikali inapata wapi fedha usipochangia wewe?” Amehoji Waziri Mwijage.
Mbali na hayo, Mwijage ametoa wito kwa wajasiriamali kuzalisha bidhaa kwa wingi na kuzingatia viwango ili kuweza kujiweka katika nafasi nzuri kwenye masoko ya nje na ndani ya nchi.
“Wakati wa kuzunguka kwenye maonyesho na bidhaa kidogo umepitwa na wakati. Mnatakiwa kuzalisha bidhaa za kutosha ili kuingia kwenye ushindani masoko ya kitaifa na kimataifa”. Amesisitiza Mwijage.