Home FEDHAMIKOPO Tanzania yaidhinishiwa mkopo wa Tsh trilioni 1.8

Tanzania yaidhinishiwa mkopo wa Tsh trilioni 1.8

0 comment 103 views

Tanzania imeidhinishiwa mkopo wenye masharti nafuu pamoja na msaada vyote vikiwa na thamani ya dola za Marekani milioni 775 sawa na Tsh trilioni 1.8.

Fedha hizo pamoja na msaada kutoka Benki ya Dunia ni kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa bajeti, kuboresha uchumi na huduma za afya.

Taarifa kutoka Wizara ya Fedha na Mipango inaonyesha mchanganuo wa fedha hizo ambapo Shirika la Kimataifa la Maendeleo (IDA) litatoa mkopo wa Tsh trilioni 1.1 kwa ajili ya kufufua uchumi ulioathiriwa na UVIKO 19 na vita baina ya Ukraine na Urusi.

UVIKO 19 na vita, vilisababisha kusinyaa kwa uchumi na kupanda kwa bei ya bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ikiwemo mafuta.

Dola milioni 250 sawa na Tsh bilioni 58 zitatumika kwa ajili ya program ya afya ya mama na mtoto kwa njia ya kupima matokeo (PfoR) inayotekelezwa Tanzania Bara.

Dola milioni 25 sawa na Tsh bilioni 58.1 zimetolewa kama msaada na Mfuko wa Dunia wa kusaidia wanawake, vijana na watoto zitatumika kwa ajili ya mradi wa uwekezaji kiuchumi (IPF) kwa upande wa Zanzibar.

“Tumekubaliana na Benki ya Dunia kwamba fedha hizo ambazo zitaanza kuingia nchini kuanzia Ijumaa, Desemba 23, 2022, zitaelekezwa katika kuiwezesha sekta binafsi kushiriki katika kukuza uchumi, kuziwezesha sekta za fedha kuwa na uwezo wa kukopesha sekta hiyo pamoja na kuimarisha uwazi na uwajibikaji serikalini.

Nyingine ni kuboresha kilimo pamoja na kutatua changamoto za afya ya mama na mtoto,” amesema Waziri wa Fedha na Mipango Mwigulu Nchemba.

Benki ya Dunia imetoa fedha za msaada wa bajeti baada ya kipindi cha miaka nane ambapo mara ya mwisho Tanzania ilinufaika na mpango huo mwaka 2014.

Hii ni baada ya kuridhishwa na utekelezaji na usimamizi wa sera za kiuchumi na kifedha, uwazi na uwajibikaji katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Katika taarifa yake, Benki ya Dunia imeipongeza Tanzania kwa usimamizi makini wa uchumi wake licha ya kuwepo kwa athari za UVIKO 19 na vita ya Ukraine na Urusi ambapo uchumi wake umeimarika na kupigiwa mfano na taasisi hizo kubwa duniani.

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter