Wakulima wa mboga kutoka Bonde la Ilolo jijini Mbeya wametoa wito kwa Halmashauri kuwawezesha kwa kuwapatia mikopo ili waweze kuongeza tija ya uzalishaji na kupata soko la uhakika kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Songwe (SIA). Wakulima hao wanaojishugulisha na kilimo cha mboga na matunda wamedai wanakumbwa na changamoto kubwa ya kukosa fedha na elimu ya fedha ambayo ingewasaidia kutimiza malengo waliyojiwekea.
Mbali na hayo, wakulima hao pia wamesema wanahitaji vifaa maalum ili kusukuma maji kutoka kwenye ardhi mpaka kwenye mashamba yao. Wakulima hao wameeleza kuwa tatizo hilo la uhaba wa maji likipatiwa ufumbuzi, watakuwa na uwezo wa kuongeza uzalishaji wao tofauti na hali ilivyo sasa.
“Kilimo cha mboga kina tija na kimesaidia kuendesha maisha yangu ya kila siku. Tukisaidiwa mitaji, elimu na miundombinu ya maji kwenye bonde hili naamini tutachangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa”. Ameeleza mmoja wa wakulima katika bonde hilo.
Kwa upande wake, Ofisa habari wa jiji la Mbeya, John Kilua amewataka wakulima hao kujiunga katika vikundi na kujisajili ili vitambuliwe kwa mujibu wa Sheria na kuweza kupatiwa mikopo itakayowasaidia kuongeza uzalishaji.