Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji ameeleza bungeni Dodoma kuwa serikali imekusanya kodi ya ongezeko la thamani (VAT) ya Shilingi bilioni 3 kwa mwaka wa fedha 2016/17 na Shilingi bilioni 2.5 kwa mwaka wa fedha 2017/18 kwenye taulo za kike zilizozalishwa nchini pamoja na zile zilizoagizwa kutoka nje ya nchi.
Akijibu swali la Mbunge Upendo Peneza (Viti Maalum Chadema) ambalo liliulizwa kwa niaba yake na Dk. Immaculate Swale (Mbunge Viti Maalum), Dk. Kijaji ameeleza kuwa, fedha hizo ni makusanyo kabla ya kodi ya bidhaa hiyo kufutwa mwezi Juni mwaka 2018.
Akiuliza swali la nyongeza, Dk. Swale amehoji hatua zinazochukuliwa na serikali kudhibiti bei ya taulo hizo ambayo inaendelea kuwa juu licha ya kufutwa kwa kodi ambapo Dk. Kijaji amefafanua kuwa hali hiyo ni kutokana na soko kuwa huru. Hata hivyo, Naibu Waziri huyo amesema serikali ipo kwenye mchakato wa kufanya utafiti wa suala hilo, na kueleza kuwa kuondolewa kwa kodi hiyo kuna manufaa zaidi kwa wazalishaji.
“Kuna nchi kama Botswana na Kenya waliondoa kodi lakini walibaini kuwa haikuleta matokeo chanya. Unapoondoa kodi kuna namna wazalishaji wananufaika. Tutajiridhisha katika tafiti tuliyoanza kuifanya na tutakuja na majibu sahihi hapa”. Amesema Dk. Kijaji.