Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Philip Mpango amesema moja kati ya vitu vinavyomnyima raha na usingizi ni pamoja na upotevu wa fedha za umma kwa kisingizio cha manunuzi. Dk Mpango amesema hayo katika maonyesho ya 42 ya biashara ya kimataifa alipozungumza na watendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kwenye banda lao la maonyesho yanayoendelea hapa Jijini Dar es Salaam.
Waziri huyo amedai fedha nyingi za umma zimekuwa zikipotea, na hivyo ameagiza kufanyika kwa utaratibu wa kudhibiti hali hiyo.
“ Ninawaagiza PPRA kuhakikisha taasisi zote za serikali zinajiunga na mfumo wa ununuzi wa umma kwa njia ya Mtandao (TANePS) ili kudhibiti na kuondoa urasimu uliokuwa ukifanyika” Alisema Dk. Mpango na kuongeza,
“ Kesho mje ofisini kwangu mniletee mpango kazi wa kulikamilisha hilo na mjiwekee muda kwa wale ambao hawajakamilisha kwa wakati waliojiwekea wachukuliwe hatua”
Dk. Mpango alisema kuwa moja ya sehemu ambayo serikali imekuwa ikiibiwa ni pamoja na ununuzi wa umma, kwa kuwa fedha nyingi zinapotea hivyo ameitaka PPRA kuzibana taasisi zote.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sheria na Uhusiano wa Umma PPRA, Betha Soka amesema tayari mfumo huo umeanza kufanya kazi kwa kuziunga taasisi 100 za umma zinazohusika na ununuzi wa vifaa tiba na dawa. Vilevile, Soka amedai kuwa, PPRA ina mpango mkakati wa miaka mitano ambao utakamilika 2019/2020.