Afya ni rasilimali muhimu ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa ubora katika shughuli za kila siku kwa mwanadamu yoyote. Bila ya kuwa na afya bora hakuna anayeweza kufanya majukumu yake ya kila siku kwa ustadi na kujiingizia kipato. Watanzania wanatakiwa kuhakikisha kuwa afya zao ni bora ili wawe katika nafasi nzuri zaidi ya kujenga taifa. Lakini haiwezekani kufanya yote hayo bila serikali kuweka msisitizo na kuimarisha huduma za afya.
Ili kuhakikisha kuwa wananchi wake wanakuwa na huduma bora za kiafya, serikali inapaswa kufanya marekebisho makubwa katika sekta hiyo. Takwimu za Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa mwaka 2016 zinaonyesha kuwa Tanzania ina jumla ya vituo 7,471 vya afya ambapo asilimia 73.7 kati ya hizo zinamilikiwa na serikali huku asilimia 26.3 zikimilikiwa na taasisi au watu binafsi. Lakini je, ubovu wa sekta hii unachangia vipi kudorora kwa uchumi hapa nchini?
Changamoto kubwa inayoikumba sekta ya afya hapa nchini ni msongamano wa watu. Watu hupoteza muda mrefu katika foleni za hospitali, jambo ambalo linapelekea shughuli za kiuchumi kukwama. Ni nini kifanyike ili kupunguza msongamano wa watu hasa katika hospitali za ngazi ya mkoa, rufaa na taifa? Nafikiri serikali ina jukumu la kuhakikisha kuwa zahanati na vituo vya afya hasa vijijini vinatoa huduma inayotakiwa ili kusudi kusiwe na haja ya wagonjwa kwenda kuhudumiwa katika ngazi za juu zaidi.
Pia, ni wajibu wa serikali kuhakikisha kuwa inaongeza idadi ya wanafunzi wanaodailiwa katika masomo ya afya ili kupata wahudumu wengi zaidi katika sekta hii hivyo kuwezesha vituo hivi kutoa huduma kwa urahisi zaidi na kupunguza mzigo kwa madaktari ambao hivi sasa wanahudumia watu wengi zaidi kuliko uwezo walionao. Dawa na vifaa tiba vipatikane kwa urahisi ili kuwezesha wataka huduma kutumia gharama nafuu na muda mfupi kuzipata.
Makampuni binafsi na yale ya serikali nayo wanatakiwa kuwajibika ili kujiridhisha kuwa wafanyakazi wake wana afya bora. Moja ya njia ya kufanya hivyo ni kuwakatia wafanyakazi wao bima za afya ili kusudi pindi mtu anapohitaji huduma za kiafya, zinakuwa rahisi kupatikana bila kuingia gharama ya malipo kwa sababu bima waliyokatiwa itagharamia mahitaji hayo yote.
Wafanyakazi pia wanapaswa kufahamu kuwa ni haki yao ya msingi kufanya kazi mahali safi na salama bila ya kuhatarisha afya zao. Mfano mzuri ni makampuni ya ujenzi. Ni wajibu wa waajiri kuhakikisha hawaweki afya za wafanyakazi wao katika hatari yoyote. Usalama katika kazi unapaswa kuwepo wakati wote. Wanaofanya kazi maeneo yenye vumbi nao wasiache kuziba pua na midomo yao kwani kufanya hivyo kunahatarisha afya zao.
Watanzania nao wanapaswa kuzingatia chakula bora. Ni muhimu kula vyakula vinavyojenga na kuupa nguvu mwili pamoja na maji ya kutosha. Jitihada za kujenga taifa haziwezi kuendelea bila kuwa na afya bora. Ni muhimu kutenga muda wa kufanya mazoezi na kupima afya zetu. Kufanya hivyo kutasaidia kugundua tatizo mapema na kupata tiba ili kuendelea na mapambano ya kufanya kazi na kupiga vita umasikini.