Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezielekeza Halmashauri zote nchini kusitisha utoaji wa fedha za mikopo kwa makundi maalum ya vijana, wanawake na wenye ulemavu kuanzia Aprili hadi Juni, 2023 wakati Serikali inajipanga kuweka mfumo mpya wa utoaji wa mikopo hiyo.
Ametoa maagizo hayo 13, 2023 Bungeni Dodoma wakati akihitimisha hoja zilizotolewa na Wabunge wakati wakijadili Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/2024.
“Katika mkutano huu wa Bunge kuliibuka hoja kuhusu kiasi kidogo cha fedha za mikopo zitokanazo na asilimia 10 ya makusanyo ya Halmashauri kinachotolewa kwa makundi maalum kutokidhi matakwa ya kuyainua makundi hayo kwa kufanya shughuli za uzalishaji au biashara.
Aidha kumekuwa na changamoto kwenye baadhi ya Halmashauri kutoa fedha hizo kwa watumishi wa Halmashauri au wakati mwingine vikundi hewa badala ya walengwa na kusababisha fedha za mikopo hiyo kutorejeshwa.
Kwa kuzingatia malalamiko hayo na maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu matumizi mabaya ya fedha hizo, nazielekeza Halmashauri kote nchini kusitisha utoaji wa fedha za mikopo hiyo zitakazotokana na makusanyo ya kuanzia mwezi Aprili hadi June 2023, wakati Serikali inajipanga kwa mfumo mpya ya utoaji wa mikopo hiyo utakaoelekezwa kabla ya mwezi June mwaka huu,” amaeeleza Waziri Mkuu.Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliagiza kuangaliwa upya kwa utaratibu wa utoaji wa mikopo ikiwemo kuangalia namna ya kutumia mabenki kupitishia mikopo hiyo wakati akipokea taarifa ya Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2021/2022 Machi 29, 2023.