Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKIUJASIRIAMALI Upigaji Picha: Jiajiri kwa kufanya haya

Upigaji Picha: Jiajiri kwa kufanya haya

0 comment 177 views

Siku zote inashauriwa kufanya kazi au kuwekeza katika vitu ambavyo tunafurahia kuvifanya, ili kupata matokeo mazuri zaidi. Hivyo kama ni mbunifu, unapenda kujifunza mambo mapya, unafurahia suala zima la picha na una vifaa vya kisasa vya kupigia picha, basi tambua kuwa unaweza kujipatia fedha kwa kufanya mambo mbalimbali mbali na kupiga picha matukio yaliyozoeleka kama harusi, wahitimu, mikutano nk.

Yafuatayo ni baadhi ya mambo ambayo unaweza kufanya na kutengeneza kipato.

Piga picha biashara ndogo

Tofauti na zamani, siku hizi ni muhimu kwa wajasiriamali na wafanyabiashara kutumia mitandao ya kijamii ili kujitangaza na kupata wateja zaidi. Wanawavutiaje wateja? Ni kupitia picha nzuri na hata video ambazo zinahitaji ubunifu na mtu mwenye uwezo na ujuzi. Hivyo kama wewe ni mpiga picha unayetaka kujipatia fedha zaidi, unaweza kuwekeza muda wako, na ubunifu wako kwa kufanya makubaliano na biashara ili kuweza kufanya nao kazi. Wafuate wamiliki wa biashara, waonyeshe kazi zako zilizopita na waeleze manufaa ya picha nzuri. Kwa mfano kama unapendelea kupiga picha za chakula unaweza kuwafuata wamiliki wa migahawa, hoteli, wauzaji wa bidhaa za vyakula, matunda nk na kufanya nao kazi.

Fundisha kupiga picha

Kila siku kuna watu ambao wanahitaji kujifunza mambo mapya, na moja kati ya fani ambazo watu hupendelea kujifunza ni kupiga picha. Hivyo kutokana na ujuzi wako unaweza kutoa huduma ya mafunzo kuhusu upigaji wa picha kwa watu mbalimbali. Kwa kufanya hivyo unafaidika na fedha, unakutana na watu wapya na wenye maarifa na uwezo mbalimbali pia unajifunza na kuongeza ufanisi.

Anzisha tovuti

Unaweza kujipatia fedha kwa kuanzisha tovuti au blog inayohusu masuala ya picha na kujipatia fedha kutokana na matangazo. Unaweza kuanzisha tovuti kuhusu tasnia ya upigaji picha, maeneo ya kupata vifaa vya kisasa vya picha kwa bei nafuu, pia unaweza kuweka picha zako na kuzielezea nk. Kadri watu wanavyoangalia machapisho yako ndio itakavyokuwa rahisi kwako kupata watu wa kutangaza huduma na bidhaa zao katika tovuti yako na kujipatia fedha. Jambo la muhimu ni kuzingatia kanuni mbalimbali za uendeshaji wa tovuti, ili kuweza kujipatia mafanikio.

Matukio

Kama unapenda kujichanganya na watu na kuhudhuria matukio, basi tambua kuwa unaweza kujipatia fedha. Kwa mfano unaweza kwenda katika sehemu za burudani na kupiga picha watu wakiwa wanafurahi kisha kuwaonyesha picha hizo kisha unaweza kuwa na bei tofauti kulingana na jinsi wahusika wanataka kuzipata picha hizo.

Kuhariri

Wapiga picha mashuhuri wanaweza kuwa na majukumu mengi na hivyo kukosa muda wa kufanya kila kazi kwa umakini zaidi. Kama una ubunifu na ujuzi wa kutosha katika upande wa kuhariri picha basi unaweza kufanya mawasiliano na wapiga picha ambao tayari wamefanikiwa na kuwaonyesha ujuzi wako wa kuhariri picha kupitia kazi ambazo umeshafanya kisha kufanya makubaliano na kupata fedha. Uzuri wa uhariri wa picha ni kuwa unaweza kufanya mahali popote.

 

 

 

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter