Home KILIMO Fahamu zaidi kuhusu kilimo cha tikiti maji

Fahamu zaidi kuhusu kilimo cha tikiti maji

0 comment 156 views

Kilimo cha tikiti maji kimekuwa kikijizolea umaarufu mkubwa hapa nchini. Wakulima wengi zaidi wamekuwa wakihamia kwenye kilimo hiki miaka ya hivi karibuni. Katika mijadala mbalimbali ya fursa za kilimo, kilimo hiki ni nadra sana kukosekana. Kama unafikiria kuingia katika aina hii ya kilimo, makala hii itakuelezea kwa undani kuhusiana na aina hii ya kilimo pamoja na faida na hasara zake.

Hapa Tanzania soko la tikiti maji ni zuri kipindi cha joto ambapo walaji wengi hupendelea tunda hili kutokana na hali ya hewa ya joto. Wauzaji wa matikiti katika masoko wanadai  kuwa biashara ya tikiti ni nzuri sana wakati wa joto na hudorora katika nyakati za baridi. Taarifa kama hizo ni nzuri sana kwa mkulima mjasiriamali anayelenga uhitaji wa soko kwani anakuwa na mipangilio mizuri katika uzalishaji wake ili asipate hasara.

Kwanza ni kilimo cha muda mfupi kwani huchukua miezi miwili hadi mitatu kiasi kwamba mkulima anaweza kulima hadi mara nne kwa mwaka mmoja. Kilimo cha tikiti maji kinafanyika katika eneo lenye udongo laini usio na mabonge kwani mbegu zake hupandwa moja kwa moja shambani. Pia shamba linapaswa kuwa katika eneo la wazi lisilo na miti sababu vivuli vya miti vinaweza kupelekea matikiti yasitoe matunda.

Uchaguzi wa aina ya mbegu ni kitu cha msingi sana katika kilimo hiki kwani shughuli zote zinajengwa kwenye msingi huo. kama ukikosea kuchagua aina ya mbegu  kilimo chako hakitakuwa na tija. Kuchagua mbegu nzuri na zenye ubora sio kazi rahisi, wakulima wengi hukimbilia mbegu maarufu ambazo zinatangazwa zaidi ambapo mara nyingi wanapokwenda kwenye uhalisia kwa kulima mbegu hizo, wanakumbana na matokeo tofauti.

Takribani asilimia tisini ya tikiti maji ni maji hivyo yanahitaji maji mengi ili kukua vizuri. Hivyo kabla ya kufanya aina hii ya kilimo, hakikisha una uhakika wa maji kipindi chote cha ukuaji. Matunda haya huitaji maji kipindi chote mpaka hatua ya uvunaji. Mizizi ya mmea wa tikiti huenda chini sana kutafuta maji kwa ajili ya kusaidia matunda yenye ukosefu wa maji. Mkulima anatakiwa kumwagilia mimea maji ya kutosha. Kama kiwango cha maji hakiridhishi basi hata matunda hayo hayawezi kukua kama inavyotakiwa.

Hasara katika kilimo cha tikiti maji hutokea kwa kiasi kikubwa kwenye kipindi cha uvunaji. Wakati huu ukifika, mkulima anakuwa na shauku kubwa ya kutaka kuonja matikiti yake ili kuona yana ladha na ubora gani. Tatizo hutokea pale inapotakiwa kutenganisha matikiti yalioiva na yale ambayo bado hayajaiva. Wengi huharibu matikiti mengi kutokana na kukosa uelewa na ujuzi wa kutenganisha makundi hayo mawili hivyo hupata hasara kubwa wakati zoezi hili likifika.

Kama unafikiria kujiajiri kupitia kilimo biashara, kilimo cha tikiti maji ni njia mojawapo ya kufanya hivyo.unaweza kulima, kuvuna na kuuza hata mara nne ndani ya mwaka mmoja hivyo kujiingizia kipato kikubwa tu. Jambo la msingi ni kuwa na uelewa mkubwa kuhusiana na kilimo hiki na kuhakikisha kuwa umejiandaa vema na umejiwekea malengo. Hakikisha pia soko lako ni la uhakika na ka kufanya hayo lazima jitihada zako zitazaa matunda.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter