Tanzania ni moja kati ya nchi zinazoongoza katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa Uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula na biashara ukilinganisha na nchi za Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi na Sudan Ya Kusini. Zipo sera na misemo kadhaa ambayo imekuwa maarufu katika kuhamasisha uzalishaji Nyanja ya kilimo kama vile ‘kilimo ni uti wa mgongo wa taifa’ siasa ni kilimo ambao ulitokana na Azimio la Iringa pamoja na Sera ya ‘Kilimo Kwanza’ Sera hizi zimefanikiwa kwa kiasi kwani zimetoa mwanya wa wakulima wadogo na wakubwa kujifunza zaidi kupitia mafunzo mbalimbali.
Lipo suala ambalo kama litatiliwa mkazo, kwa kiasi kikubwa litachangia uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula na malighafi mbalimbali yatokanayo na kilimo.
Umewahi kujiuliza kuhusu kupima au kutambua aina ya udongo wa shamba na mazao yanayofaa kulimwa katika shamba lako? Jibu hili laweza kuwa ndio au hapana. Basi ni muhimu sana kutambua na kujua aina ya udongo uliopo katika shamba lako na aina ya mazao yanayoweza kufaa kwa kulima katika eneo hilo. Serikali imekuwa ikihamasisha watu kuchukua udongo wa mashamba yao kwa ajili ya vipimo vya maabara ili kujua kiasi cha asidi iliyopo katika udongo, rutuba pamoja na aina ya mazao yanayostahili kulimwa katika eneo hilo. Zipo maabara mbalimbali nchini Tanzania ambazo zimekuwa zikitumika kupimia udongo kama vile Maabara ya Uyole Mbeya, Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine pamoja na mawakala mbalimbali wa pembejeo nchini wakiwemo Yara pamoja na Syngenta. Ni vema kabla ya kuendelea ukapata ufahamu wa kujua kwanza nini fasili ya udongo
Aina za udongo na sifa zake
Kuna aina tofauti za udongo. Aina zote ni mchanganyiko wa aina nne za chembechembe za madini: kichanga, mchangatope,tifutifu na mfinyanzi. Kemikali zinazounda chanzo cha punje za udongo na jinsi punje hizi tatu zinavyounganishwa huamua aina ya udongo uliopo. Husaidia kujua sifa bainifu za msingi za udongo, iwapo udongo una asidi, alikali au hauna kitu chochote. Aina tofauti za udongo ni kama ifuatavyo: Udongo wa kichanga, udongo wa mchangatope, na udongo wa mfinyanzi.
- Udongo wa kichanga
Udongo wa kichanga huundwa kutokana na kuvunjika vunjika na kumomonyoka kwa miamba kama vile mawe ya chokaa, matale, mawe meupe ya kungaa na mwambatope. Udongo wa kichanga una punje kubwa ambazo zinaonekana kwa macho, na kwa kawaida zina rangi za kungaa. Udongo wa kichanga huonekana kuwa na chenga ukiloweshwa au mkavu na hauminyiki unapouminya kwenye kiganja. Udongo wa kichanga hunyumbuka kwa urahisi na huruhusu unyevu kupenya kwa urahisi, lakini hauwezi kuuhodhi kwa muda mrefu. Huzoea haraka hali ya joto. Maji kupenya kwa urahisi huzuia matatizo ya kuoza mizizi. Udongo wa kichanga huruhusu maji kupitiliza zaidi ya kiasi kinachohitajika, ambayo husababisha mimea kukosa maji wakati wa kiangazi. Kwa hiyo iwapo mtu atapanda mimea katika udongo wa kichanga, itabidi kutegemea chanzo cha kudumu cha maji wakati wa kiangazi. Udongo wa kichanga una mboji kidogo sana na kwa kawaida una asili ya asidi. Kwa baadhi ya mazao kama peasi, ambayo huhitaji udongo wenye hali ya alikali ili uweze kutoa maua na kubeba matunda, kuna haja ya kuzimua hali ya asidi kwa kuongeza chokaa au kaboneti ya kalsiam kila mwaka ili kuendeleza hali inayofaa kwa kilimo. Udongo wa mchanga huathirika kwa urahisi na mmomonyoko hivyo inahitaji kukingwa dhidi ya upepo na mvua. Kupatikana kwa mboji mara kwa mara huboresha kwa kiwango kikubwa uwezo wake wa kuhifadhi maji na virutubisho, pia na uwezo wa kuzuia mmomonyoko. Matandazo pia husaidia udongo wa mchanga kuhodhi unyevu kupitia kupungua kwa mvukizo kutoka kwenye udongo. - Mchangatope
Mchangatope ni udongo wenye chenga ndogo zaidi kuliko udongo wa mchanga hivyo ni laini unapoushika. Udongo huu ukimwagiwa maji, unateleza kama sabuni. Unapoufi nyanga kati ya vidole vyako, unaacha uchafu kwenye ngozi. Mchangatope unapatikana katika maeneo asilia au kama tope katika tabaka kwenye maziwa, mito na bahari. Huundwa na madini kama vile mawe angavu ambayo yana madini aina ya kwatzi na punje ndogo ndogo za mabaki ya viumbe hai. Ni chengachenga kama udongo wa mchanga lakini unahodhi virutubisho vingi zaidi na unyevu. Unatengeneza gamba kwa urahisi juu ya udongo, ambalo huzuia maji kupenya na unaweza kuzuia mimea isichomoze. Katika hali ya unyevu, hupenyeza maji kwa urahisi na ni rahisi zaidi kulima. Kadri mabaki ya viumbe hai yanavyokuwa mengi, ndivyo inavyonyonya maji ya mvua vizuri zaidi na kuendeleza muundo wake hata baada ya mvua kubwa, hivyo kuzuia mmomonyoko. - Udongo mfinyanzi
Udongo mfinyanzi huundwa na chembe chembe ndogo sana ambazo zina sehemu ndogo sana ya kupitisha hewa. Udongo mfinyanzi huundwa baada ya miaka mingi ya miamba kumomonyoka na athari za hali ya hali ya hewa. Pia hutengenezwa kama mashapo yaliyotua baada ya mwamba kupasuliwa vipande vipande na hali ya hewa, kumomonyolewa na kusafi rishwa. Udongo mfinyanzi kutokana na mchakato wa uundwaji wake unakuwa na madini mengi sana. Udongo mfinyanzi unateleza na kunata unapokuwa mbichi lakini laini unapokauka. Udongo mfinyanzi huhodhi unyevu vizuri, lakini haupenyezi maji vizuri, hasa unapokuwa mkavu. Mara nyingi vidimbwi hutokea kwenye udongo mfinyanzi na udongo hugandamizwa kwa urahisi. Kutokana na uwezo wake mdogo wa kupenyeza maji, hatari ya maji kutuama na ardhi kuwa ngumu, sio rahisi kufanya kazi na udongo mfinyanzi. Kuongeza mboji na jasi huboresha hali ya udongo na kuufanya kulimika kwa urahisi. Jasi na mboji hutenganisha chembe chembe za udongo mvinyanzi na hivyo kuruhusu maji kupenya na kuhodhiwa kwa usahihi. Kuongeza mabaki ya viumbe hai kwenye udongo hukuza kuongezeka kwa minyoo ya ardhini, ambayo husaidia kuinua ubora wa udongo. - Udongo tifutifu
Udongo tifutifu hutengenezwa na uwiano mzuri wa mchanga, mchangatope, mfi nyanzi
na mabaki ya viumbe hai. Huchukuliwa kama udongo unaofaa zaidi katika ardhi inayolimika. Udongo tifutifu una rangi nyeusi na unafanana na kushika unga mikononi. Umbile lake ni mchanga mchanga na huhodhi maji kirahisi sana, hata hivyo upenyezaji wake wa maji ni mzuri. Kuna aina nyingi za udongo tifutifu kuanzia wenye rutuba hadi ulio na tope zito na tabaka nene la juu. Hata hivyo kati ya aina zote hizi tofauti za udongo, udongo tifutifu ndio unaofaa zaidi kwa kilimo.
Kwanini unashauriwa kupima udongo wa shamba lako?
-Kupima udongo kunasaidia kujua aina ya zao linalofaa kwenye shamba lako
-Kwa kupima udongo utajua virutubisho ambavyo viko kwenye udongo na kwa kiasi gani
-Kupima udongo kuna punguza gharama kwani utanunua mbolea kulingana na upungufu rutuba ya udongo wako, wakulima wengi wamekuwa wanatumia mbolea hata kwa mashamba ambayo virutubisho viko vya kutosha na pia kutasaidia kutunza mazingira kwasababu baazi ya virutubisho vikizidi kwenye udongo huweza kuharibu mazingira.
-Kupima udongo kutakusaidia kujua mahitaji kamali ya mbolea/virutubisho
-Kupima udongo kutakusaidia kujua jinsi ya kuuboresha udongo kwa kuweka chokaa au jasi, hii ni baada ya kujua pH ya udongo.
-Kupima udongo kutakusaidia kujua zao gani upande
-Kupima udongo kutakusaidia kujua utumie mbolea gani na kwa kiasi gani.
Wataalamu wa kilimo wanashauri kupima udongo kila baada ya miaka mitatu. Taasisi binafsi, jumuiya, serikali, wadau wa kilimo na mashirika mbalimbali ya kilimo yana wajibu mkubwa wa kuhakikisha yanatoa elimu, semina, warsha pamoja na makongamano yanayohusiana na kilimo cha kisasa ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa elimu kuhusiana na umuhimu wa upimaji wa udongo.