Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga amesema Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) unapaswa kununua mahindi ya kutosha kutoka kwa wakulima ili kuongeza wigo wa masoko kwa wakulima wa mazao mbalimbali ya nafaka hapa nchini. Hasunga amesema hayo alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na kuongeza kuwa, ni wakati wa NFRA kubadilisha dhana ya kununua mahindi kwa ajili ya hifadhi pekee, na badala yake wanatakiwa kununua mahindi kwa ajili ya kuuza ili kuongeza ufanisi wa soko kwa wakulima nchini.
Aidha, Waziri huyo pia amesema kuwa tayari NFRA imeshaanza kutekeleza maelekezo ya serikali kwa kununua na kuuza mahindi kupitia mkataba na Mpango wa Chakula Duniani (WFP). Wakala huo pamoja na Bodi ya Nafaka na Mazao mchanganyiko wametakiwa kutekeleza wajibu wake katika kufanya biashara ya mazao.
Pamoja na hayo, Hasunga ametoa wito kwa watanzania wote kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuleta maendeleo.