Kutotoa vifaranga ni uwekezaji mzuri na mafanikio katika uwekezaji huu hurudi kwa haraka. Biashara hii haihitaji ujuzi mkubwa sana, na wauzaji wa mashine za kutotolea vifaranga hutoa maelekezo ambayo humsaidia mfugaji kufanya biashara hii na kupata mafanikio.
Kwa Tanzania, asilimia 70 ya uzalishaji wa vifaranga hufanywa kwa njia ya asili kwa kutumia kuku wa kienyeji.
Na ndio maana watanzania wengi wanapendelea zaidi kuku wa kienyeji, jambo ambalo linasababisha mahitaji ya kuku hao kuwa makubwa hivyo kusababisha bei ya kuku wa kienyeji kuwa kubwa sokoni.
Watanzania wengi sasa wanaacha kula nyama nyekundu na kula zaidi nyama nyeupe kwasababu za kiafya. Hii inatokana na ushauri wanaopata kwa madaktari kuhusu madhara ya nyama nyekundu hivyo wengi wao sasa wanatumia zaidi kuku na samaki.
Kutokana na sababu tatu, ambazo ni mahitaji makubwa ya kuku wa kienyeji, kuacha kuingizwa kuku wa kisasa nchini na umuhimu wa nyama nyeupe kwa wananchi kuna kila sababu ya kuanzisha biashara hii ya utotoaji na mfanyabiashara hatojutia.
Kutokana na mashamba mengi ya kutotoa na kufuga kuku kuwa katika maeneo ya makazi na wafanyabiashara wengi kukosa nyaraka kutoka kwa madaktari wa mifugo, na wao wenyewe kutokuwa wamejisajili katika sehemu husika wafanyabiashara wengi hupata hasara pale kuku wakifa kutokana na sababu tofauti.
Hivyo ili kuondoa changamoto hii, ingefaa wafanyabiashara wanaotaka kufanya biashara hii kuhamasishwa kujisajili katika maeneo husika, na kuwepo kwa mustakabali unaoeleza kanuni na kuwaongoza watu wanaotaka kufanya biashara hii pia kuwepo taasisi itakayokuwa inafuatilia masuala yote ya kuku kuanzia mayai, nyama yake na mbolea pia.
152